Mbunge ataka Waziri, watumishi wote utalii wafutwe kazi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki

DODOMA; Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, amesema ni vyema Bunge likaweka rekodi kwa kuwafukuza kazi watumishi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sababu wamewadharau kutokana na manyanyaso kwa wananchi wanaoishi pembeni mwa hifadhi.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2024/24, Mbunge Mpina amesema wananchi wanaokaa kandakando ya hifadhi wamekuwa wakinyanyaswa kupigwa na kuonewa na kwamba aliwahi kuwasilisha ushahidi kuhusu kutekwa na kuuawa baadhi ya wananchi na Waziri Mkuu alitoa maagizo kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Amesema hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuhusu watumishi wanaonyanyasa raia na kuwabambikia kesi

Advertisement

“Kitendo cha Wizara ya Maliasili na Utalii kukaa kimya, Waziri Mkuu ametoa maagizo yakapuuzwa, wewe (Spika) umeniagiza nilete ushahidi hakuna kilichotekelezwa, kamati mpaka sasa inaripoti hakuna kilichofanyika.

“Sasa kwa sababu wote tumedharauliwa, naomba kulishauri Bunge lifanye yafuatayo. Moja waheshimiwa wabunge tumuombe… naomba waheshimiwa wabunge  leo tutoe fundisho tuitake Serikali kupitia Waziri Mkuu kuwafukuza kazi watumishi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzia Waziri mpaka mfagizi wa ofisi,” amesema Mbunge Mpina.