Mbunge atwishwa kero za hospitalini Mpanda

WAJAWAZITO Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wameeleza kusikitishwa na namna wanavyodaiwa vifaa vya kujifungulia ikiwemo mipira (gloves) na vitu mbalimbali wakati wa kujifungua, huku wakidai kutohudumiwa endapo watakosa vifaa hivyo.

Hayo yamebainishwa na Hamisa Mongomongo pamoja na Nasra Ibrahimu kwenye mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi katika Kata ya Nsemulwa, wakati akisikiliza kero za wananchi.

Kwa nykati tofauti wananchi hao wameeleza Serikali kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikisisitiza utoaji huduma bila malipo hasa kwa wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano, lakini hali imekuwa tofauti kwao pindi wanapokwenda kupata huduma hizo.

“Utakuta naagizwa mipira 10 halafu natumia mipira mitatu,ile saba inayobaki inakwenda wapi? Kama nimeinunua mwenyewe basi nina haki ya kurudishiwa mipira yangu nikaiuze,” amesema Nasra Ibrahimu.

Akijibu hoja hiyo, Kaimu Mganga Mkuu Manispaa ya Mpanda, Erick Kisaka amesema vifaa hivyo ni kwa ajili ya maandalizi ya kujifungulia kwa kuwa mipira inayotolewa na serikali haitoshelezi, huku akifafanua huduma zinazotolewa bure kwa wajawazito na watoto.

“Nitoe wito, kwenye vituo vya serikali ikatokea umeenda ni mjamzito au umempeleka mtoto¬† chini ya miaka mitano ukahitajika kutoa hela, hilo ni suala ambalo litakuwa ni kinyume na utaratibu na mnaweza mkatoa taarifa ili mtu yule achukuliwe hatua,” amesema.

Kwa upande wake Mbunge Kapufi amesema suala hilo atalifanyia kazi, lakini pia amesisitiza kukubaliana na maelekezo ya wataalamu kwa kuwa faida kubwa inarudi kwa wananchi.

Pia mbunge huyo amewaomba wananchi kuendelea kuiamini serikali, kwani inaendelea kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya afya ili manufaa zaidi yaweze kupatikana.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button