Mbunge Kabati aja na Make Iringa Digital

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati (CCM) ameunadi mkakati wake wa ‘Make Iringa Digital’ unaolenga kuziwezesha shule zote za sekondari za serikali mkoani humo kuwa na maabara ya kompyuta na kufungwa mfumo wa TEHAMA.

Mkakati huo kwa mujibu wa mbunge hyo umejielekeza katika kuharakisha mageuzi makubwa ya matumizo ya teknolojia hiyo kwa wanafunzi, mkoani Iringa.

Ametoa taarifa hiyo leo aliposhiriki kongamano la klabu ya ICT-RUCU ya Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha cha mjini Iringa.

Advertisement

“Napenda niwaambie wana jumuiya ya ICT-RUCU kuwa mnaishi katika ndoto zangu katika kuhakikisha Iringa unakuwa mkoa wa mfano kwa matumizi ya TEHAMA kuanzia shuleni hadi katika taasisi na ofisi mbalimbali ili kuleta mabadiliko na kuboresha utendaji,” alisema.

Katika kutimiza lengo hilo Kabati alisema mradi wa Make Iringa Digital umepata wadau kutoka nchini Marekani watakaosaidia kufunga mfumo wa TEHAMA katika shule za sekondari za mkoa huo.

“Tayari mradi huo umeanza hatua za utekelezaji katika shule za sekondari za wilaya ya Kilolo ambako tumekwishaanza kupeleka kompyuta kwa ajili ya kuunganishwa na mifumo ya TEHAMA,” alisema.

Katika kongamano hilo klabu ya ICT- RUCU imemuomba mbunge huyo kusaidia kuishughulikia changamoto ya upatikanaji wa mtandao wa WIFI na vifaa vya kitaalam katika kupakua na kuweka mifumo mbalimbali ndani ya chuo hicho, maombi ambayo Kabati ameyapokea kwa utekelezaji.

Klabu ya ICT- RUCU inajumuisha wanafunzi wote wanaosoma katika kitivo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada.