Mbunge kuwapa raha wasanii Nsimbo

MBUNGE wa Jimbo la Nsimbo, Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, Anna Lupembe amedhamiria kuwaunganisha wasanii wa muziki wa kizazi kipya na muziki wa ngoma za asili wa jimbo hilo katika Mfuko wa Taifa wa Utamaduni, ili waweze kunufaika na mikopo ya fedha itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Amesema hayo wakati wa hafla ya bonanza la kuibua vipaji vya sanaa ya muziki katika Kijiji cha Tumaini Kata ya Itenka, Halmashauri ya Nsimbo ambapo ameeleza nia yake ya kukuza michezo mbalimbali pamoja na sanaa.

Lupembe amesema kuwa kupitia bonanza hilo ameona vipaji mbalimbali jinsi, jambo ambalo limemvutia na kuona namna bora ya kuwaunga mkono waweze kukua zaidi kwenye sanaa hiyo.

“Tumecheza ngoma na tumeona vipaji mbalimbali hapa, ndugu zangu vikundi vyote vya ngoma mliojiandikisha mlioimba hapa ninawaingiza kwenye kundi la mfuko wa utamaduni wa taifa, tutakuja kufanya usajili na BASATA itakuja kuwasajili na kuanza kupewa mikopo,” amesema Lupembe.

Lupembe amesema kwa mwaka huu ameweza kuhamasisha sanaa ya utamaduni maarufu kama ‘mbina’ au ‘matanda’ ambayo itafanyika mwezi Septemba na kujumuisha makundi ya sanaa ya jimbo lote la Nsimbo.

“Sanaa ni ajira ambayo kama itathaminiwa na wadau mbalimbali itaweza kukua zaidi katika mkoa wetu wa Katavi na pia kuingizwa kwenye mfuko wa Taifa wa utamaduni sio tu utawawezesha wasanii kupata mikopo ya kifedha, bali ni lango la wasanii kutambulika kitaifa,” amesema Maria Nyango kiongozi wa kikundi cha ngoma ya asili Sumu ya Mamba.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button