MKUU wa Gereza la Liwale mkoani Lindi , David Mkobya ameshukuru Mbunge wa Jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka kwa kuwapatia wafungwa na mahabusu msaada wa magodoro 20 .
Mkobya ambaye ni Mrakibu wa Jeshi la Magereza, aliyasema hayo jana ofisini kwake wakati akipokea msaada huo ulitolewa na mbunge Kuchauka ambaye alifanya ziara katika gereza hilo na kutoa msaada huo.
Gereza hilo lina uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 105 kwa mafungio ya jana lilikuwa na wafungwa na mahabusu 76 na kwamba gereza halina msongamano.
” Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Lindi , napenda kutoa ashukurani zangu za dhati kwa msaada huu uliotupatia, kwani wafungwa na mahabusu nao ni binadamu nao wanaitaji kupatiwa misaada mbalimbali kama hii na pia nawaomba na wadau wengine katika jamii wajenge utamaduni wa kutoa misaada kwa mahabusu na wafungwa, ” alisema SP-Mkobya.
Pia SP- Mkobya alisema gereza lina changamoto ya udhaifu wa ngome ya gereza ambayo ni ya miti na inashambuliwa na wadudu mara kwa mara, uchakavu wa jiko la kisasa la gereza kwa ajili ya kupikia chakula cha wafungwa na mahabusu,kutokamilika kwa jengo la utawala.
Kwa upande wake Kuchauka alisema amesikia changamoto hizo na kwamba atahakikisha anazifikisha katika uongozi wa ngazi za juu, ili ziweze kutatuliwa kwa haraka na akapongeza gereza hilo kwa kutokuwa na msongamano wa mahabusu na wafungwa gerezani.