MBUNGE wa Jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz Abood amewataka vijana waendesha pikipiki ( bodaboda ),kuanzisha vikundi na kuvisajili ili wanufaike na mikopo ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya maendeleo yao.
Abood alisema hayo Januari 23,2023 wakati alipotembelea maeneo mbalimbali ya vituo vya kazi vya Bodaboda na kuwakabidhi zawadi za majaketi yenye viakisi mwanga (Reflector Jackets) zipatazo 1,500 yakiwa na ujumbe : “ Sisi na Mama “ na “Tanzania The Royal Tour”.
Mbunge huyo alisema hatua hiyo ni jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan pamoja na yeye (Mbunge ) katika hatua ya kuliepusha kundi hilo kubwa na ajali barabarani hususani nyakati za usiku.
Abood alisema madereva wa bodaboda ni kundi kubwa , hivyo wakijiunga kwenye vikundi na kuvisajili watakuwa na uhakika wa kunufaika na fursa za mikopo ya asilimia nne (4) kwa vijana inayotolewa na halmashauri ili kuendeleza kipato chao kitakachowainua kiuchumi .
“ Serikali ya awamu ya sita imetoa fursa nyingi za uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake , vijana na watu wenye ulemavu , nina waomba vijana tumieni fursa hii , azisheni vikundi vya bodaboda visajilini ili kupata mikopo hii ambayo haina riba “ alisema Abood
Alisema kupitia mikopo watakayoipata watakuwa na uwezo wa kununua pikipiki za kikundi vyao na kuendeleza mitaji itakayowaongezea kupata mafanikio makubwa ya kijamii na kiuchumi.
“ Azisheni vikundi mimi mbunge wetu nipo tayari kuwasaidia kuvisajili , tumieni fursa zinazotolewa na Rais wetu kwani wanawapenda wananchi wake “ alisema Abood
Kuhusu zawadi za majaketi ( Reflector Jackets) Mbunge huyo alisema licha ya kuwalinda katika usalama wao pia zina yamebeba ujumbe wa kuitangaza Tanzania na filamu ya The Royal Tour kwa vile wanakutana na watu wa aina mbalimbali wakiwemo raia wa kigeni na hivyo kufikisha eneo kubwa.
Kwa upande wa madereva hao akiwemo , Ally Yusuph wa Kituo kikuu cha Msamvu cha Mabasi yaendayo mikoani alimshukuru Rais pamoja na Mbunge huyo kwa jitihada zao za kulijali kundi hilo .
Yusuph alisema. madereva wengi wa bodabodas wamefariki dunia kwa kugongwa n magari kutokana na kukosa viasiki mwang hivyo na upatikanaji wake kwao kutasaidia kupunguza ajali barabarani hasa nyakati za usiku na pia kuahidi kutangaza utalii.