Mbunge Mwambe atoa ushauri minada ya korosho

MBUNGE wa Jimbo la Ndanda, mkoani Mtwara Cecil Mwambe ameshauri serikali kuondoa baadhi ya tozo kwenye zao la korosho, ili kumuwezesha mkulima kuuza na kupata faida katika minada inayoendelea nchini.

“Mimi sioni dalili za kupanda kwa korosho sana sana itashuka kwa sababu ‘supply’ imekuwa kubwa. Nashauri serikali iridhie kuachana na tozo zinazotozwa kwenye zao la korosho, ili mkulima abakiwe na pesa ya faida mara baada ya kuuza ,” amesema.

Kauli ya Mwambe imefuatia hatua ya wakulima mikoa ya Lindi na Mtwara kukataa kuuza korosho zao katika minada kwa msimu wa 2022/2023 kwa madai kuwa bei iliyotangazwa ni ndogo kuliko gharama za uzalishaji.

Minada hiyo ilianza Jumamosi Oktoba 22, 2022 katika sehemu mbalimbali za Lindi ya Mtwara, huku bei ya juu ikiwa ni  Sh 2,200 na chini Sh 1,480.

Mwambe amesema gharama za uzalishaji ni wastani wa shilingi 1,470  ambapo tozo ni zaidi ya sh 300 na kwamba wakulima wakiuza kwa bei ya Sh 2,200 bei ya juu na ya chini Sh 1,480 watapata hasara kwenye gharama za awali za uzalishaji.

Mbunge huyu amesema wakulima wanakataa kuuza kwa sababu watapata hasara kutokana na gharama za uzalishaji kuwa kubwa kulinganisha na bei ya kuuza.

Habari Zifananazo

Back to top button