Mbunge Shangazi aulizia Barabara Kwekanda– Hekicho – Mkomazi

DODOMA; SERIKALI imesema katika mpango wa bajeti mwaka 2024/25, imetenga Sh milioni 313, ili kukamilisha uwekaji wa changarawe, tabaka la zege barabara ya Kwekanda – Hekicho – Mkomazi, Jimbo la Mlalo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Zainab Katimba, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaka kujua ni lini Serikali itakamilisha kuweka changarawe katika barabara inayounganisha tarafa za Umba, Mlalo, Mtae ya Hekicho, Lugurua hadi Manolo.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Katimba amesema: ‘’Maeneo yanayotajwa na Mheshimiwa Mbunge yapo katika barabara ambayo imesajiliwa kwa jina la Kwekanda – Hekicho – Mkomazi yenye urefu wa kilomita 20.5 inayounganisha tarafa za Umba, Mlalo, Mtae ya Hekicho, Lugurua hadi Manolo.’’

Advertisement

Amesema Serikali imeendelea kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe pamoja na kujenga miundombinu ya kupitisha maji ya mvua, ambapo mwaka 2021/2022, Serikali ilitumia Sh milioni 500 kuifungua ili iweze kupitika.

“Aidha, katika mwaka 2022/2023, Sh milioni 201.5 zilitumika kujenga vivuko 14 vya maji, kuweka changarawe kilomita 8.0 na tabaka la zege mita 80 kwa baadhi ya vipande vyenye miinuko mikali.

“Ndani ya mwaka 2023/24 Sh milioni 328 ilitumika kwenye uwekaji wa changarawe kilomita 7.2, tabaka la zege mita 110 na kujenga vivuko 5 vya maji.Mpaka sasa jumla ya kilomita 15.2 zimeshawekwa changarawe.

“Katika mpango na bajeti wa mwaka 2024/25, Serikali imetenga Sh milioni 313 ili kukamilisha uwekaji wa changarawe, tabaka la zege mita 200, kujenga vivuko 7 vya maji ambapo barabara hiyo itaweza kupitika katika kipindi chote cha mwaka,” amesema.