MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameahidi kuharakishwa kwa mchakato wa kufunguliwa maduka ya Kariakoo kwa saa 24.
Chalamila amesema hatua hiyo inakuja siku chache baada ya serikali kuruhusu mabasi ya mikoani kusafiri saa 24.
Amesema hayo leo mkoani Dar es Salaam kwenye bonanza la michezo kati ya Mamlaka ya Mapato(TRA) na wafanyabiashara wa Kariakoo.
Uamuzi huo wa mabasi kusafiri saa 24 ulitolewa Juni 29 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akiahirisha shughuli za Bunge jijini Dodoma.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema, awali walikuwa wamejipanga kufanya biashara saa 24 baada ya kumalizika kwa ujenzi wa soko la Kariakoo Oktoba mwaka huu.
Lakini kutokana na uamuzi huo wa mabasi kusafiri saa 24, ameona kuna haja ya kuharakisha mpango huo kwa kuanza kukesha mapema.
“Itakuwa ni aibu sana watu wanatoka mkoani usiku wanafika Dar na kutukuta tumefunga maduka,hivyo tutahakikisha tunaanza kufungua maduka saa 24 haraka iwezekanavyo na hivi karibuni tutaanza hata kwa majaribio,” amesema.
Akizungumzia kuhusu bonanza hilo Chalamila amewapongeza TRA kwa kulifanya kwa kile alichoeleza kuwa linasaidia kuwaweka pamoja wafanyabiashara na TRA.
“Niwapongeze TRA kwa kuandaa bonanza hili kwani limewaleta pamoja na wateja wenu niwaombe muandae pia na maeneo mengine mliyoyatenga kimkakati kwani itakuwa ni fursa ya kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi,”amesema.
Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya TRA, Alphayo Kidata, amesema mashindano hayo yamehusisha tawi la mkoa wa kimkakati wa kikodi Kariakoo na watumishi wao wa TRA.Ametaja michezo ambayo wameshindana kuwa ni mpira wa miguu, netball, ķuvuta kamba na kufukuza kuku.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara,Martin Mbwana.amesema bonanza hilo ni mwanzo mzuri wa husiaono kutokana na waliyopitia hivinkaribuni.
Mbwana aliahidi wataendelea kuhamasishana kulipa kodi bila shurti kwakwa kuwa sio jambo la mtu binafsi bali ni la nchi na ndizo zinazowezesha kuleta maendeleo katika nchi.