“Mchakato wa hisa kampuni ya madini uharakishwe”

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka Wizara ya Madini kuharakisha mchakato wa kumiliki hisa ya asilimia 37 kutoka kwenye Kampuni ya Williamson Diamond Ltd inayochimba madini ya almas Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Kwa taarifa waliyopewa kamati hiyo mpaka sasa mgodi huo wa almas unaumiliki wa asilimia 75 na ukomo wa leseni ya uchimbaji mwisho mwaka 2033 huku Serikali ya Tanzania ikimiliki hisa kwa asilimia 25.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shabani Ng’enda ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma alisema hayo jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea mgodi huo na kuhitimisha huku wakiitaka wizara hiyo kuendelea kusimamia mgodi kwa ukaribu .

Ng’enda alisema kuhusu huduma ya jamii (CSR) mgodi huo unatakiwa utoe mapato ghafi ya asilimia 0.7 huku akipongeza jitihada za kutoka kulipa shilingi Milioni 300 hadi Sh bilioni 1.2. fedha zitokanazo na mapato ghafi.

“Sasa hivi kamati hii tunatoa ushauri kwa Serikali kufanya mapitio na tathimini upya pamoja na mchakato wa ulipwaji fidia ili kuondoa malalamiko ya chinichini kwa wananchi walio athiriwa na bwawa tope.”alisema Ng’enda.

Ng’enda alisema wameona ulipwaji wa fidia umeenda vizuri kwa kuwajengea nyumba zenye thamani kubwa waathirika kuliko walizokuwa nazo awali za tope nakuishauri serikali kuangalia uwezekano wa kutomboa nyumba hizo ziweze kupata milango ya dharura ambayo haikuwekwa.

Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa alisema kuhusu Serikali kumiliki hisa asilimia 37 katika mgodi huo lipo kwenye mchakato wa mazungumzo baina ya Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na uongozi wa juu wa umiliki wa mgodi huo.

Diwani wa kata ya Mwadui Lohumbo Francis Manyama alipotakiwa na kamati hiyo kueleza CSR wanavyoipata alisema kata yake ina vijiji vinne na vyote vimezungukwa na mgodi ambapo kila kijiji kinapata mgawo wa Sh milioni 80 nakuweza kujenga shule.

Mhandisi mkuu wa mgodi huo, Shaghembe Mipawa akimwakilisha meneja mkuu, Ayoub Mwenda alisema ushauri wamepokea na kampuni ina utaratibu mzuri wa kupokea malalamiko na kamati inataka yapatiwe majibu,nyumba ziongezwe milango na CSR itolewe kwa mujibu wa sheria.

Habari Zifananazo

Back to top button