Mchanganuo tozo zilizofutwa, zilizopunguzwa

SERIKALI imetangaza marekebisho katika tozo za miamala ya kielektroniki kutoka benki Kwenda kwenye simu na mawakala wa benki na ATM.
Akizungumza leo bungeni Dodoma leo, Septemba 20, 2022 katika kipindi cha Maswali na Majibu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema marekebisho yaliyofanyika ni kufuta tozo za kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote) tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja, tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine na kusamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha.
Mchanganuo wake:
Kwa mujibu wa Waziri Mwigulu, serikali imesamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi Sh 30,000.
Serikali imepunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kufuatana na kundi la miamala.
“Ikumbukwe kuwa tozo hizo viwango vilishushwa kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu cha Sh 10,000 hadi kiwango cha juu cha Sh 7,000,” amesema.
Dk Mwigulu amesema marekebisho hayo yataanza kutumika Oktoba Mosi, mwaka huu.
Hatua hiyo ya serikali imekuja baada ya wananchi na makundi mbalimbali kuibuka na kulalamikia tozo hizo, CCM iliitaka serikali iandae utaratibu wa kupitia upya sera na Sheria ya Kodi na kuratibu ubunifu utakaoibua vyanzo vipya vya kodi ili kupunguza mzigo kwa wananchi.