Mchango wa madini maduhuli ya serikali waongezeka

TUME ya Madini katika mwaka 2022/2023 imepata mafanikio makubwa yakiwemo ya kukusanya maduhuli ya serikali ya Sh bilioni 678.04 kutoka Sh bilioni 624.61 zilizokusanywa katika mwaka 2022/2022 na makusanyo hayo ni sawa na asilimia 82.49 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 822.02.

Akizungumza jijini hapa jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume, Ramadhani Lwamo alisema ongezeko hilo limetokana na usimamizi mzuri wa tume hiyo. Lwamo alisema pia mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuongezeka kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini.

Kwa mujibu wa Lwamo, mwaka 2022 mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa ulikuwa asilimia 9.1 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo ulikuwa asilimia 7.2. Pia ukuaji wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 9.6 mwaka 2021 hadi asilimia 10.9 mwaka 2022.

Advertisement

“Tunaamini tutaweza kufikia mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa wa asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM 2020 na Dira ya Maendeleo ya Taifa,” alisema Lwamo.

Tume ya Madini kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imefanikiwa kuanzisha jumla ya masoko ya madini 42 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 94 nchini.

Lwamo alisema serikali ilianzisha masoko ya madini tangu Machi 17, 2019 kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa biashara ya madini nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini kwa serikali.

Katika mwaka 2022/2023, masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilichangia jumla ya Sh bilioni 157.42 kama mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini sawa na asilimia 23.22 ya makusanyo yote yaliyokusanywa na tume kwa mwaka husika.

Katika kuendelea kuimarisha uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini, mwaka 2022/23, tume ilitoa leseni 9,642 kati ya leseni 9,174 zilizopangwa kutolewa. Kati ya leseni zote zilizotolewa, 6,511 sawa na asilimia 70.97 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo na kudhihirisha azma ya serikali ya awamu ya sita kuendeleza wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika sekta ya madini.

Tume imefanikiwa pia kufanya ukaguzi katika masuala ya usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini kwenye migodi midogo 19,580 iliyopo katika mikoa ya kimadini. Katika ukaguzi huo yalibainika baadhi ya mashimo kutofukiwa, matumizi hafifu ya vifaa kinga na vilipuzi na wahusika walielezwa kufanyia kazi upungufu huo kwa kuzingatia Sheria ya Madini Sura namba 123.

Imetoa pia mafunzo kwa wachimbaji madini kuhusu masuala ya usalama, afya, mazingira pamoja na usimamizi wa baruti kwa wachimbaji wadogo wa madini katika mikoa ya Singida, Dodoma, Mara na Kigoma. Mwelekeo wa Tume kwa mwaka 2023/2024 ni kuhakikisha mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama ilivyofafanuliwa ndani ya Dira ya Maendeleo, Ilani ya CCM pamoja na Mpango Mkakati wa Tume wa 2019/20-2023/24.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *