WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, ametoa mwezi mmoja kwa Baraza la Michezo nchini (BMT) kuweka mfumo wa kielektroniki kusajili wanachama wake.
Mchengerwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 27, 2022 katika ufunguzi wa mashindano ya mpira wa miguu ya wanawake yanayojulikana kama Mpira Fursa katika vyuo vya maendeleo (FDCs).
Michuano hiyo inaratibiwa na Taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).
“Natoa mwezi mmoja kwa BMT kusajili taasisi zote za michezo kwa njia ya mtandao, achanen na analogia,” amesema Mchengerwa na kuongeza:
“Usajili ni siku moja, haiwezekani mtu yupo Ngara mpaka aje physical na bado atatumia siku tatu nne, dunia imebadilika na nyie mbadilike, mkishindwa kufanya hivyo nitawaondoa,” amesema.
Mchengerwa, ameipongeza KTO kwa kuwa na programu ya michezo kwa vyuo vya maendeleo, shule za sekondari na msingi na kwamba itasaidia mkakati wa serikali wa kukuza soka nchi.
“Tumechoka kuwa vichwa vya mwendawazimu, lazima tujipange lazima tuwe na mpango mkakati kujiandaa kucheza kombe la Dunia mwa 2030.
“Tunajiandaa kwa miaka nane, atakaetukwamisha tutamtoa, hatuwezi kufanya vizuri kwa kuleana, kila wakati tunaenda tunapigwa nyundo tatu tunarudi sasa basi, imetosha, serikali ipo tayari kushirikiana na kutoa sapoti yote katika kukuza soka letu lengo ni kuona tunapiga hatua,’ amesema.
Awali akizungumzia programu ya KTO, Mia Mjengwa amesema KTO inawawezesha wasichana mbalimbali ambao wamekatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito, mbali na kuwasaidia kujiendeleza katika vyuo vya maendeleo pia wanakuza vipaji vyao katika fan mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu.
Amesema kupitia programu hiyo, imewawezesha wasichana 11 kupata mafunzo ya ukocha chini ya TFF na wengine 11 wanatarajiwa kuanzia mafunzo hayo.