Mchengerwa atoa maagizo ujenzi wa soko Bukoba

KAGERA: Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ametoa maagizo kwa uongozi wa Mkoa wa Kagera na Manispaa ya Bukoba kuhakikisha hawakwamishi utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa soko la kisasa utakaoanza kutekelezwa kwa mwaka wa Fedha 2024/2025.

Ametoa maagizo hayo alipotembelea soko kuu la wafanyabiashara wa Manispaa ya Bukoba na kuwahakikishia kuwa kupitia Mradi wa uboreshaji wa miundombinu mbinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) kwa miji 15 kundi la pili Bukoba wanaenda kunufaika na soko la kisasa lenye hadhi ya kimataifa kama la Kariakoo Dar es salaam.

Amesema ili mradi huo uweze kutekelezwa haraka uongozi wa Manispaa ya Bukoba na Mkoa wa Kagera wanapaswa kujiandaa kuanzia sasa na kuandaa eneo zuri la wafanyabiashara kuhamia ili kuendelea kufanya biashara zao na kulipa kodi wakati utekelezaji ukiendelea.

“Tunaweza kupata mkandarasi haraka ,fedha haraka lakini mradi ukakwamishwa na kutojipanga ,naomba kuanzia sasa tujue wapi wafanyabiashara wanahamia kabla ya mradi kuanza kutekelezwa,biashara haipaswi kusimama ,kodi ziendelee kulipwa huku mradi wa soko ukiendelea kukamilishwa sitegemei ukwamishaji wala malalamiko “amesema Mchengerwa.

Amesema kuwa mradi huo uzingatie kuwapitia maeneo wafanyabiashara wote walionyanganywa maeneo sokoni kipindi cha Nyuma,wafanyabiashara wapya,waliopo ,wanaopanga bidhaa nje ya soko na wote wapate nafasi katika soko jipya litakalojengwa.

Amewahakikishia wafanyabiashara wote ambao wanataka nafasi katika soko jipya kuwa watapata nafasi na kuwaeleza kuwa dhamira ya Raisi Samia ni kubadilisha hadhi ya Manispaa ya Bukoba na kuwa mji wa kisasa unaovutia huku akikemea wale wote ambao wanapanga kufanya ubadhilifu kuwa serikali haitafikiria mara mbili kuwaondoa .

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Amid Njovu akitoa taarifa kwa Waziri wa TAMISEMI amesema kuwa kwasasa soko kuu linawafanya biashara wapatao 1,400 huku wananchi wapatao 10,000 wakifaya manunuzi  ya bidhaa mbalimbali kwa siku katika soko hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kuwa tayari mkoa na manispaa wamejipanga kupokea mradi huo na wameanza kufanya maandalizi ya kuwahamisha wafanyabiashara kwa kutafuta eneo rafiki la kuhamia na kuendelea kufanya biashara kwa uhuru.

 

Habari Zifananazo

13 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button