WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji wa wizara yake kuwatumia askari waliohitimu mafunzo ya awali ya kijeshi kuhakikisha wanatatua tatizo la wanyama wakali wanaovamia makazi ya watu na kusababisha madhara ikiwemo vifo na kuharibu mazao.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali kwa askari 231 kutoka TFS na NCAA, katika kituo cha mafunzo ya jeshi la uhifadhi Mlele mkoani Katavi, ambapo amesema askari hao wakafanye kazi ya kuwarudisha hifadhini wanyama hao, kabla hawajapangiwa vituo vyao vya kazi.
“Kama tunavyowahimiza wananchi kuondoka kwenye maeneo ya hifadhi na sisi tunapaswa kutimiza wajibu wetu, nikuagize Katibu Mkuu kuhakikisha kwamba wanyama hao wanaondoshwa na kurejeshwa maeneo yao,”amesema Mchengerwa.
Amewataka askari hao kutumia vizuri ujuzi na weledi walionao kuhakikisha wanasimamia vizuri rasilimali za nchi kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo.
Naye Kamishina wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dosantos Silayo, amesema changamoto wanazokutana nazo ni kuongezeka kwa matishio ya usalama kwa askari kipindi wanatekeleza majukumu yao.
Pia amesema kuna uvamizi mkubwa wa maeneo ya hifadhi kwa wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu, kama vile kilimo na ufugaji.
Wakati akisoma risala kwa mgeni rasmi mmoja wa wahitimu Mwita Magoiga, amesema kituo hicho cha mafunzo kinakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara, inayotokea Mpanda kuelekea kambini Mlele, hali inayosababisha kuacha vipindi na kuanza kukarabati barabara, ili kusafirisha vyakula na mahitaji ya kambini.
Nao baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo, wakizungumza kwa nyakati tofauti wameahidi kufanya kazi kwa bidii, ikiwemo kulinda rasilimali za nchi na kupambana na wanyama wakali wanaovamia makazi ya watu, ili kuokoa maisha na mali za wananchi.