WAZIRA wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amesema ili wizara hiyo iongeze zaidi pato la taifa, lazima kuwe na mabadiliko ya lazima ya kuondoa kanuni za hovyo zinazoleta vikwazo kwa wadau wa utalii.
Mchengerwa amesema hayo leo Jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Uhifadhi wa Wanyama Pori, Misitu na Nyuki na kusema kuwa yeye ni mtendaji katika wizara hiyo na anataka kuona sekta zote zilizopo katika wizara yake zikiwajibika na kuongeza pato la taifa kutoka asilimia 21 hadi asilimia 33.
Alisema katika sekta ya nyuki, Tanzania ni ya pili Afrika kwa kuuza asali nje ya nchi ambapo inauza Dola milioni 12 kwa mwaka.
Amesema kuwa kiasi hicho ni kidogo kwani aliwataka wadau wa sekta hiyo kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kiwango hicho kinapanda na kufika Dola milioni 50 au 100.
Mchengerwa amewataka watendaji wa sekta hiyo kuwasilisha changamoto zao kama zipo ili serikali iweze kuzifanyia kazi kwa maslahi ya wadau wa sekta hiyo na serikali.
Waziri Mchengerwa aliwataka wadau kuwa na Imani na serikali yao kwani anafanya kazi saa 24 kwa maslahi ya nchi na yuko tayari kuwasikiliza na kuzitatua changamoto.
” Wizara yangu haitaki mawazo binafsi bali inataka mchango wa mawazo ya jumla yenye kuboresha wizara kwa ujumla hususan katika sekta zote hivyo nataka muwe wazi bila woga kwa maslahi ya nchi” amesema Mchengerwa
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abas amesema amefurahishwa kukutana na wadau wa sekta ya wanyamapori, misitu na nyuki na kusema kuwa baada ya mkutano huo huenda sekta hizo zitachangia zaidi pato la taifa.