Mchengerwa: ‘Sitakuwa na uvumilivu’
DART yatakiwa kuongeza watoa huduma
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ameuelekeza Uongozi wa Wakala wa Mabasi ya Mwendokasi (DART) kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri wa haraka kwa wananchi wa Dar es Salaam
Mchengerwa ameyasema hayo kwenye ziara yake kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART)
Aidha, amewataka watendaji wa DART watoke kwenye utendaji wa kimazoea na wafanye kazi na kwamba hataki kusikia watu wakilalamika kutumia muda mwingi vituoni.
Mchengerwa amesema kumekuwa na changamoto inayotia dosari dhamira njema ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi kusimama muda mrefu vituoni.
“Sitaki nisikie kuna mabasi yametelekezwa, yarekebishwe mabasi yote yaingie kutoa huduma.
“Ndoto za Rais watanzania wawe na furaha, watumiaji mwendo kasi wawe na furaha wasibugudhiwe.
“Msimamie mtoa huduma UDART kelele zimekua nyingi hatutaki watu wababaishaji, hawafuati ratiba na kusababisha mrundikano vituoni
Mwendokasi iwe chini ya nusu saa.
“Tumezoea kufanya kazi ndani ya box, mkiletewa bajeti hiyo hiyo inatosha, mipango mingi mizuri mataifa mengi yanakuja kuchukua mipango yetu wanaenda kutekeleza kwa vitendo wanafanya vizuri zaidi sisi tunabaki na malalamiko,”amesema Mchengerwa na kuongeza
“Sasa namtaka Mtendaji Mkuu (Edwin Mhede) kila mmoja kujiandaa kutoka kwenye ‘comfort zone’, kama mlizoea kufanya kazi kwa kurithika tu, upo ofisini unajizungusha kwenye kiti huku watu wanalalamika vituoni, sitakuwa mvumilivu, na sitegemei kulisikia.
Mchengerwa ameagiza Wakala kuandaa na kutekeleza mpango wa kuwa na mabasi yanayojitosheleza njia zote ili mpango wa ratiba usibadilike.
Pia ameagiza Mabasi yaliyoharibika yote yarekebishwe na kwamba hataki kusikia kuna mabasi yaliyoharibika.
“Ongezeni umakini katika kumsimamia mtoa huduma UDART kelele zimekua nyingi hatutaki watu wababaishaji katika kutoa huduma
“Tunataka mtu ambae ana uwezo wa kutoa huduma bila kuwepo malalamiko, nawaagiza angalieni uwezekano wa kupata mtoa huduma zaidi ya mmoja hasa katika njia mpya ya Mbagala
“Hatutaki mtoa huduma mwenye maringo au asiye na mtaji wa kutosha, angalieni uwezekano wa kupata watoa huduma zaidi ya mmoja.”Amesema
Amesema, kukiwa na Kampuni zaidi ya moja ya kutoa huduma kutakua na ushindani, lakini watoa huduma wote watashirikiana na serikali.. akitolea mfano Mbagala kuna watu wengi hivyo akipatikana mwekezaji goigoi ataleta malalamiko kwa wananchi.