Johannesburg, Afrika Kusini; MCHEZAJI wa Afrika Kusini na timu ya Kaizer Chiefs Luke Fleurs, ameuawa kwa kupigwa risasi katika tukio la utekaji nyara wa gari Johannesburg, Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika timu yake, tukio hilo la risasi lilifanyika katika kituo cha mafuta usiku wa kuamkia leo katika kitongoji cha Johannesburg, Florida.
Msemaji wa polisi huko Gauteng, Luteni Kanali Mavela Masondo, amewaambia waandishi wa habari kwamba tukio hilo lilitokea wakati mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 24 akiwa anasubiri kuhudumiwa, ndipo ghafla alivamiwa na watu wasiojulikana wakiwa na silaha, wakamwamuru ashuke nje ya gari.
“Washukiwa walimtoa nje ya gari lake, kisha wakampiga risasi moja sehemu ya juu ya mwili wake,” ameeleza Luteni Kanali Masondo.
Kauli kutoka kwa Kaizer Chiefs, wamesikitishwa na tukio hilo lililosababisha kifo cha mchezaji wao, huku wakidai polisi wanashughulikia suala hilo na taarifa zaidi zitawasilishwa kwa wakati unaofaa.
Fleurs alijiunga na Kaiser Chiefs mwaka jana akitokea timu ya SuperSport United ya nchini humo.
Katika tovuti yake, Kaiser Chiefs imeeleza kwamba Fleurs alikuwa beki wa kiwango cha juu na ni fundi mno”.
Alianza kucheza soka mwaka 2013 alipokuwa Chuo cha Ubuntu Cape Town, Mashabiki wa soka wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii wakiombolea kifo chake.