Mchezo wa manati wachangia adha ya umeme Mtwara

Mchezo wa manati wachangia adha ya umeme Mtwara

VITENDO vya watoto wilayani Masasi, Mtwara kulenga vikombe vilivyopo kwenye nguzo za umeme kwa kutumia manati ni miongoni mwa sababu mbalimbali zinazochangia tatizo la umeme katika maeneo hayo likiwemo jimbo la Lulindi, Bunge limefahamishwa.

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema hayo Bungeni leo asubuhi wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Lulindi, Issa Mchungahela aliyetaka kujua muda ambao Serikali itamaliza tatizo la umeme mkoani Mtwara hususani wilaya ya Masasi na Jimbo la Lulindi.

Akieleza sababu nyingine, Naibu Waziri amesema umeme mdogo usiotosheleza (Low Voltage) kwenye baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo kwa sababu ya umeme kusafiri umbali mrefu; uchakavu wa miundombinu hasa nguzo na vikombe pamoja na uharibifu kwenye miundombinu ya njia ya kV132 unaotokana na watoto kupiga manati vikombe katika baadhi ya maeneo.

Advertisement

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Bunge limeelezwa, ili kuondoa tatizo hili Serikali kupitia TANESCO imetengwa Shilingi
bilioni 2 ili kujenga njia kutoka Nanganga hadi Masasi.

“Aidha, ufungaji wa Auto Voltage Regulator (AVR) mpya yenye ukubwa wa MVA 20 kati ya Tunduru na Namtumbo unaendelea ili kuwezesha umeme wa kutosha kutoka Ruvuma kufika Masasi na maeneo
ya jirani,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa kutumia Shilingi milioni 600, Serikali inaendelea kubadili vikombe vilivyopasuka (kuweka vya plastiki) na nguzo za miti zilizooza zinabadirishwa.
Mbunge huyo hakukubaliana na sehemu ya jibu la Naibu Waziri hususani suala la vikombe kuharibiwa kwa manati na kuitaka Serikali kufanya utafiti zaidi.

Kuhusu ufumbuzi wa kudumu, Byabato amesema Serikali imepanga kuunganisha mkoa wote wa Mtwara na Gridi ya Taifa kupitia miradi miwili ya Gridi Imara ambayo ipo katika hatua ya utekelezaji. Miradi hii ni ujenzi wa njia kuu ya umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru na kutoka Tunduru hadi Masasi.