Mchina mbaroni kudanganya kuibiwa mil 60/-
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemkamata mhasibu katika Kampuni ya Kichina ya Your Choice’, Deodatus Lubela kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ameibiwa Sh milioni 60 alizozitoa benki.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro alisema jana ofisini kwake kuwa mtuhumiwa huyo ambaye jina lake maarufu ni baba Banzi, Novemba 14 mwaka huu saa 8:30 mchana alifika Kituo cha Polisi Chang’ombe na kusema aliporwa Sh milioni 60 ambazo alizitoa Benki ya CRDB Tazara.
Kamanda Muliro alisema mtuhumiwa huyo alidai fedha hizo alitumwa na kampuni hiyo azichukue benki akiwa na hundi tatu za Sh milioni 20 kila moja.
“Akiwa mita 100 kutoka benki anasema kuwa alikutana na majambazi ambao walimnyang’anya fedha hizo na kumtupa eneo la njiapanda ya Mbezi na Pugu,” alisema.
Kamanda Muliro alisema makachero walitumwa kuchunguza taarifa hizo kwa kuwa walizitilia mashaka ingawa mtuhumiwa huyo alikutwa na majeraha kwenye mkono wa kushoto na shavu la kulia.
Alisema baada ya kuhojiwa ilibainika taarifa alizotoa mtuhumiwa zilikuwa za uongo.
“Baada ya majadiliano zaidi mtuhumiwa alikiri kuwa fedha hizo alizodai zimeporwa alikwenda kuzificha eneo la Chanika kisha alichukua bisibisi na kuanza kujijeruhi. Pesa zote ambazo alidai kuporwa alionesha na zimepatikana,” alisema Kamanda Muliro na kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo.
Katika tukio linguine, alisema wamemkamata Joseph James (32) akituhumiwa kujifanya Ofisa Polisi wa Upelelezi kutoka Makao Makuu Dodoma.
Kamanda Muliro alisema James aliwakamata watu ovyo na kuwaingiza mahakamani, baadaye kuomba fedha ili mahakama iwaachie.
Alisema James na wenzake wakati wakifanya udanganyifu huo wamekuwa wakitumia gari lenye namba za usajili na T550 DCT ambalo walilitumia na kupita maeneo mbalimbali.