Mchinjita atwaa fomu kugombea makamu mwenyekiti

WAZIRI Kivuli wa Nishati kutoka chama cha ACT Wazalendo Isihaka Rashidi Mchinjita leo Februari 16, 2024 amechukuwa fomu kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Machi 5, 2024.

Mchinjita ambaye pia ni Ujumbe wa Kamati ya ACT amesema lengo lake ni kuimarisha ngome za chama hicho ili kuzifanya kuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wa Tanzania kupigania haki na ustawi wa taifa.

“Ni maoni yangu kuwa imani yangu isiyo na shaka katika harakati za kupigania demokrasia yenye kujenga taifa la wote kwa maslahi ya wote huu ni wakati sahihi kwangu kushiriki kikamilifu katika uongozi wa harakati hizi muhimu kwa taifa letu,”amesema Mchinjita.

Mchinjita ameeleza kuwa shauku yake ni kuimarisha sera na mwenendo wa chama hicho ili kibaki kuwa chama kinachosimama kama chama kiongozi kwenye kusukuma na kushinikiza utekelezaji wa agenda zenye maslahi kwa wananchi.

“Ni tamaa yangu kukijengea chama changu uwezo wa kuendelea kuwa chama chenye kuibua masuala na kuonesha masuluhisho ili hatimaye wananchi wakiamini na kukiwezesha kuunda serikali,”

Aidha ni azma yangu kushirikiana na viongozi na wanachama wenzangu kuwa na chama kitakachoweza kuweka shinikizo madhubuti ili kuhakikisha rasilimali za taifa letu, mipango yetu ya uchumi inajenga Taifa la wote kwa maslahi ya wote.” Ameongeza Mchinjita.

Habari Zifananazo

Back to top button