Mchungaji afariki katika mfungo akiusia atafufuka

JESHI la Polisi mkoani Geita limethibitisha kifo cha mchungaji, Abdiel Raphael (42) mkazi wa Mtaa wa Uwanja, Kata ya Nyankumbu mjini Geita, aliyefariki akiwa katika maombi na mfungo wa siku nane.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Safia Jongo ametoa taarifa hiyo leo alipozungumuza na waandishi wa habari na kueleza mchungaji huyo alikutwa na umauti Desemba 3, 2022 akiwa ndani kwake.
Amesema marehemu alikuwa na kanisa nyumbani kwake na wakati akiingia katika maombi na mfungo, aliwaaminisha waumini wake endapo wataona amefariki wasiwe na shaka kwani atafufuka.
“Mpaka ilipofika tarehe nane wanaendelea na maombi, lakini akawa hafufuki, ilipofika tarehe 9, na ile hali ya mwili kuendelea kuharibika, ndipo walipoamua kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa.
“Na kweli madaktari walipomfanyia uchunguzi wakakuta huyu mtu alikuwa ameshakufa kwa siku nyingi sana, na alivyofanyiwa uchunguzi akakutwa chanzo cha kifo chake ni kutokula kwa muda mrefu.
“Alikuwa anawaaminisha waumini wake kwamba anao uwezo wa kufa na kufufuka, anao uwezo wa kuishi bila kula kama Yesu (Kristo) na bado akafa na akafufuka.”