Mchungaji mbaroni tukio la ushirikina

MCHUNGAJI kiongozi wa Kanisa la Pentekoste Gospel Mission, Emanuel Karata (35) na mwenzake mmoja anayefahamika kwa jina la Basenga Matheo (59) wameshikiliwa na jeshi la polisi mkoani Pwani kwa kutengezeza tukio la kishirikina la kuanguka na ungo kanisani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, ACP Pius Lutumo alisema kuwa watu hao wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Advertisement

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 24 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi kwenye kanisa hilo, ambapo Matheo aliahidiwa ujira wa Sh 50,000 kutekeleza tukio hilo ili kuongeza waumini na lengo la mchungaji na mtuhumiwa huyo ni kupata waumini zaidi kwa ajili ya kuongeza kipato.

Alisema kuwa Matheo alianguka na ungo na vifaa vyake vya kishirikina akiwa na wenzake sita wakati akisafiri kishirikina na kudondoka kanisani hapo jambo ambalo lilileta taharuki kubwa kwa waumini.

Aidha Kamanda alisema kuwa baada ya uchunguzi walibaini kuwa tukio hilo ni la kutengeneza kwa lengo la kuwalaghai na kuwaadaa waumini na wananchi.

“Hata hivyo baada ya mahojiano Matheo alijinasibu kuwa alifika kanisani hapo ili kupima imani ya waumini hao kwa Mwenyezi Mungu na kuahidiwa kiasi hicho baada ya kutimiza ulaghai huo,”alisema Lutumo.

Alitoa onyo kwa watu wenye tamaa ya kupata kipato kwa haraka kwa kufanya ulaghai na kuacha mara moja na kuwataka waumini kuwa makini na watu hao wanaotaka kuharibu imani za kidini kwa tamaa ya kipato.

5 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *