MCT yafanya jambo huduma za maktaba

BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limekabidhi zaidi ya nakala 300 za machapisho matano ya vitabu vyenye thamani ya Sh milioni 8.9 kwa Bodi ya Maktaba Tanzania kwa ajili ya Watanzania wanaotumia huduma za maktaba kujiongezea maarifa.

Machapisho hayo ya vitabu yenye maudhui tofauti, yalikabidhiwa leo kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Maktaba (TLSB), Mboni Lusekela na Mkurugenzi wa MCT, Kajubi Mukajanga, ili watumiaji wa huduma za maktaba wajifunze kuhusu taaluma ya uandishi wa habari.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ukumbi wa Maktaba Kuu Dar es Salaam, Mukajanga alisema vitabu hivyo ni sehemu ya utaratibu wa MCT kutoa machapisho mbalimbali kuhusu weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Wiki nne zilizopota tulizindua machapisho manne, ambayo tunataka tukabidhi nakala zake kwa maktaba pamoja na chapisho moja la nyuma,” alisema Mukajanga.

Alitaja vitabu hivyo kuwa ni State of the media in Tanzania 2020/2021, ambacho kinaelezea hali ya vyombo vya habari nchini, Mwongozo wa vyombo vya habari wa kuandika habari za watoto, Kitabu cha kufundishia masuala ya jinsia kwa vyuo vya habari, Mwongozo wa sheria ya upatikanaji wa habari na Taarifa ya Uhuru wa vyombo vya habari.

“MCT kwa kushirikiana na wadau tulifanya marejeo ya mtaala, tukaingiza masomo mapya ambayo yalikuwa ni Vyombo vya Habari na Jinsia na Uandishi wa Habari za Data, tumeona baadhi ya wakufunzi hawana uzoefu na masomo hayo ndiyo sababu tukaamua kuandaa mwongozo wa kufundishia na kwa kuanza tumeanza na mwongozo wa kufundishia habari za jinsia,” alisema.

Akitoa salamu za shukrani Mkurugenzi wa TLSB, alisema machapisho hayo ni muhimu na wao katika majukumu yao watahakikisha wanayatunza, kwa ajili ya vizazi endelevu, ili vinufaishe wengi zaidi na aliishukuru MCT kwa kutambua umuhimu wa TLSB katika kuwapa taarifa Watanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button