MCT yakabidhi Bodi ya Maktaba vitabu 300

Baraza la Habari Tanzania (MCT), limekabidhi zaidi ya nakala 300 za machapisho matano ya vitabu vyenye thamani ya Sh milioni 8.9 kwa Bodi ya Maktaba Tanzania, Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga jana alikabidhi machapisho hayo kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Maktaba (TLSB), Mboni Lusekela na ili watumiaji wa huduma za maktaba wajifunze kuhusu taaluma ya uandishi wa habari.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba Kuu Dar es Salaam, Mukajanga alisema vitabu hivyo ni sehemu ya utaratibu wa MCT kutoa machapisho kuhusu weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

“Wiki nne zilizopota tulizindua machapisho manne ambayo tunataka tukabidhi nakala zake kwa maktaba pamoja na chapisho moja la nyuma,” alisema.

Mukajanga alitaja vitabu hivyo kuwa ni State of the media in Tanzania 2020/2021 ambacho kinaeleza hali ya vyombo vya habari nchini, mwongozo wa vyombo vya habari wa kuandika habari za watoto, kitabu cha kufundishia masuala ya jinsia kwa vyuo vya habari, mwongozo wa sheria ya upatikanaji wa habari na taarifa ya uhuru wa vyombo vya habari.

Alisena MCT waliona pia kuna umuhimu wa Watanzania kuielewa vizuri sheria ya upatikanaji wa habari na waliamua kuitafsiri katika lugha rahisi ili kila mmoja aielewe na aitumie kwa usahihi.

Alisema kwa kufikisha vitabu hivyo katika maktaba kutasaidia kuwafikia watanzania wengi wanaotumia huduma za maktaba na kuwapatia maarifa kuhusiana na taaluma ya Uandishi wa habari popote ambako huduma hiyo inapatikana.

Akitoa salamu za shukrani Mkurugenzi wa TLSB alisema Machapisho hayo ni Muhimu na wao katika majukumu yao watahakikisha wanayatunza kwa ajili ya vizazi endelevu ili vinufaishe wengi zaidi na aliishukuru MCT kwa kutambua umuhimu wa TLSB katika kuwapa taarifa watanzania.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button