Mdee, wenzake wambana Dk Lwaitama

MAWAKILI wa Mbunge Halima Mdee na wenzake 18 wameanza kuwahoji maswali ya dodoso mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Chadema, Profesa Azaveri Lwaitama.

Dk Lwaitama alionekana kukerwa na kutokuwa na utayari wa kujibu maswali aliyoulizwa.

Hayo yalijiri jana mbele ya Jaji Cyprian Mkeha katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu wakati wa kusikilizwa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wabunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdee na wenzake.

Profesa Lwaitama alikuwa akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa wakili wa wabunge hao, Ipilinga Panya na alionekana kukwepa kila swali aliloulizwa.

Profesa Lwaitama alidai kuwa alijiunga na Chadema mwaka 2015 akiwa ni mwanachama wa kawaida hadi mwaka Mei 11, 2022 alipoombwa kushika nafasi ya Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini.

Profesa Lwaitama alikiri kuapa kiapo kinzani na kusaini ingawa katika maelezo yake alidai alisaini baada ya kusomewa na kueleweshwa na mwanasheria kilichomo ndani ya kiapo hicho lakini hakushiriki kuandaa.

“Mimi siyo mwanasheria, sina utaalamu wa kuandaa, iliandaliwa nikaeleweshwa nikaelewa nikasaini,” alidai.

Alipoulizwa kutokana na kiapo anawatambuaje Mdee na wenzake, alikwepa kuwataja kama wabunge na badala yake alichukua dakika kadhaa akibishana na wakili Panya na baadaye akawataja kwa namna isiyo ya moja kwa moja.

“Mheshimiwa naweza kusema waliapishwa kana kwamba wao ni wabunge, kwa sababu haiwezekani kuwa wabunge kama chama hakijawateua naweza kusema walitamkwa tu kuwa wabunge,” alidai.

Pia alieleza kuwa anakerwa na kitendo cha wabunge hao kuendelea kuwepo bungeni wakati hawastahili.

Katika shauri hilo, wabunge hao pamoja na mambo mengine, waliiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza uanachama, kisha itoe amri tatu.

Amri ya kwanaza, wabunge hao wanaomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama, mbili, iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza na tatu itoe amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.

Habari Zifananazo

Back to top button