Mechi tatu za unyama AFCON

WATEMI Cameroon, Nigeria, Misri, Ghana wameshindwa kutamba katika michezo yao ya kwanza ya ufunguzi Mataifa ya Afrika.

Misri imeambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Msumbiji, Cameroon 1-1 dhidi ya Guinea, Nigeria 1-1 dhidi Equtorial Guinea, kisha Ghana akakutana kipigo cha mabao 2-1 kutoka Cape Verde.

Matokeo hayo yanafanya ugumu wa kujua mwelekeo wa timu za kundi A, B,C kwa kuzingatia ugumu wa michezo yenyewe na matokeo ambayo yanaendelea kushangaza watu.

Advertisement

Baada ya matokeo hayo, sasa kuna mechi tatu ambazo zitaamua hatma ya wakongwe, waliotajwa hapo juu, na mechi hizo huenda pia zikawa ni kisasi.

CAMEROON vs SENEGAL

Senegal itamenyana na Cameroon katika pambano la hadhi ya juu kati ya wababe wawili kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Ijumaa jioni.

Ulikuwa mwanzo mzuri wa kutetea taji la AFCON kwa Simba ya Teranga baada ya ushindi wa mabao 3-0 Gambia. Hii ni mechi ya uzito ambayo itaamua mwelekeo wa vigogo wa kundi C.

Kinachovutia zaidi katika mchezo huu, Cameroon itahitaji kushinda mchezo huo, ili kufufua matumaini ya kusonga 16 bora, pia bingwa mtetezi Senegal anahitaji ushindi kujihakikisha hatua inayofuata.

IVORY COAST vs NIGERIA

Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Guinea-Bissau kwenye mchezo wa ufunguzi, Ivory Coast wanatazamia kushinda mechi zao zote mbili za ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya CAF kwa mara ya kwanza tangu 2013.

Baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Equatorial Guinea, Nigeria itahitaji kupata ushindi ili kufufua matumaini ya kosonga 16 bora. Ivory Coast wamepoteza mchezo mmoja tu kati ya mechi 38 za mwisho za hatua ya makundi AFCON (W23 D14).

Nigeria wamepoteza mchezo mmoja tu kati ya mechi 12 zilizopita za hatua ya makundi ya AFCON (W8 D3).

Faida waliyonayo Ivory Coast kwanza ni mashindano hayo kufanyika katika ardhi ya nyumbani, lakini pia wataingia kwenye mchezo huo wakijiamini baada ya kushinda mchezo wa kwanza. Kwa upande wa Nigeria nguvu kubwa itakayotumika kwanza kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kufufua matumaini.

GHANA vs MISRI

Wasakana waonana, unyama ni unyama tu, mtoto kapewe wembe kazi kwake, mechi ya kisasi, mechi ya Afrika, mechi ya Dunia.
Misri imepoteza mechi moja tu kati ya 20 za mwisho za hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (W14 D5), na kufungwa 1-0 na Nigeria mwaka 2022.

Kufuatia sare ya 2-2 na Msumbiji kwenye mchezo wa kwanza, Mafarao hao watajaribu kuepuka aibu ya kufungwa ili kusonga mbele. Ghana alipokea kichapo cha 2-1 kutoka kwa Cape Verde. Black Stars haijapoteza mechi zao mbili za kwanza katika mashindano tangu 1984, ikipoteza kwa Nigeria na Algeria.

Achana na hizo rekodi kinachovutia zaidi hapa, mara kadhaa Ghana amekuwa mnyonge mbele ya Misri na ndio maana tunasema mechi ya kisasi. Katika mechi tano za mwisho walizokutana Ghana imeshinda mara moja dhidi, imepoteza mara tatu na sare moja.

Kinachovutia zaidi Ghana wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza fainali ya AFCON dhidi ya Misri mwaka 2010 ambapo walipoteza bao 1-0 lililofungwa na Mohammed Nagy ‘Gedo’ dakika za jioni na Misri kuwa mabingwa.

Mchezo huo utakuwa wakuvutia ambapo utapigwa kesho saa 5 usiku.