Mechi ya Machifu, Wabunge yaja

TIMU ya soka ya Machifu inatarajiwa kuchuana na Wabunge Mei 27, mwaka huu Uwanja wa Jamhuri, Dodoma mchezo wa kuchangia fedha kwa ajili ya wagonjwa wa saratani walio katika hali ngumu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Julius Mwaiselege, amesema mchezo huo umeandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, kwa lengo la kukusanya Sh milioni 300 kwa ajili ya kusaidia wagonjwa 100 wa saratani, walioko kwenye mazingira magumu.

Amesema licha ya mchezo huo, lakini pia kuanzia Mei 25-28 kutakuwa na tukio la uchunguzi wa awali wa magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo saratani mkoani Dodoma na kutaja baadhi ya saratani zinazoongoza kuwapata watu wengi ni saratani ya mlango wa kizazi, matiti, mfumo wa chakula, ngozi, na tezi dume.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Anton Sangalali kutoka mkoani Simiyu, amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kubaini wagonjwa wengi wa saratani hawana msaada na wengine hupoteza maisha kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa.

Naye Mjumbe kutoka Barberian, Ghazyaan Nassoro ambaye kwa kiasi kikubwa pia amechangia kuanzishwa kwa mkakati huo amesema ujumbe huo umekuwa ukishirikiana na Umoja wa Machifu Tanzania kwa muda mrefu katika shughuli mbalimbali, hivyo kwa ushirikiano mkubwa watahakikisha suala hilo linafanyika.

Ametoa wito kwa wananchi, sekta binafsi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchangiaji huo, ili kusaidia wa wagonjwa wa saratani kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button