MERCK FOUNDATION: Jamii isiwanyanyapae wasioweza kuzaa

JAMII imeshauriwa kuacha tabia ya kuwatenga watu wasio na uwezo wa kupata watoto hatua itakayowaepusha kuondokana na magonjwa yatokanayo na msongo wa mawazo yanayosababishwa na hali hiyo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Merck Foundation, Seneta Dk Rasha Kelej wakati wa mkutano wa siku mbili uliowakutanisha baadhi ya wake wa Marais wa Afrika, Wataalamu wa Afya pamoja na Waandishi wa habari Jijini Dubai- UAE hivi karibuni.

Dk Rasha ambaye kupitia Taasisi yake, amekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na unyanyapaa kwa watu wasio na uwezo wa kupata watoto alisema kuwa jamii ikibadilisha mtazamo hasi dhidi ya watu wasio na uwezo wa kupata watoto itawapatia furaha na amani watu hao.

“Jamii inapaswa kutambua kuwa kukosa mtoto au kutokuwa na uwezo wa kupata mtoto ni tatizo linaloweza kuwakuta watu wote yani wanawake kwa wanaume na siyo lazima iwe ni tatizo mwanamke peke yake,” amesema.

Advertisement

Hivyo kwa maana hiyo wote wanapaswa kuwa na faraja itakayowawezesha kujiona bado ni sehemu ya jamii na ni wenye kustahili kupata ushauri utakaowawezesha kukabiliana na changamoto hiyo.”

Kwa upande wake Mke wa Rais wa Malawi, Monica Chikwera akizungumza kwa niaba ya wake wa marais wa Afrika walioshiriki mkutano huo alibainisha kuwa wanawake wasiokuwa na uwezo wa kupata watoto wamekuwa ni waathirika wakubwa zaidi wa unyanyapaa hatua inayowakosesha fursa mbalimbali za kiuchumi hivyo serikali imekuwa ikiwawezesha kwa kuwapatia mikopo nafuu kuwasaidia kujiendeleza kimaisha.

Taasisi ya Merck Foundation tangu mwaka 2017 imekuwa ikitekeleza mradi wa More than a Mother ambao umelenga kuwasaidia wanawake kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya.