ARGENTINA itakabiliana na Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia keshokutwa, huku Lionel Messi na Kylian Mbappe wakivutia mataifa yao kuelekea kwenye fainali hizo.
Je, michuano hiyo itakumbukwa kama ‘Kombe la Dunia la Messi’ kama Argentina itabeba ubingwa au Mbappe ataiongoza Ufaransa kulibeba kombe mara mbili mfululizo baada ya kulibeba miaka minne iliyopita Urusi?
Ifuatayo ni makala kutoka BBC Sport ikizungumzia wachezaji wengine sita waliokuwa vinara kwenye kuongoza nchi zao kwenye mafanikio miaka ya nyuma.
Pele, Brazil – 1958
Pele alikuwa na umri wa miaka 17 pekee Brazil ilipokwenda kwenye Kombe la Dunia mwaka 1958 nchini Sweden, ikionekana itashinda kombe hilo kwa mara ya kwanza.
Aliachwa kwenye kikosi katika mechi mbili za mwanzo kisha mshambuliaji huyo akacheza katika mechi ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Soviet Union na kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Wales kwenye robo fainali.
Kuanzia hapo, hakuzuilika. Alifunga ‘hat-trick’ katika ushindi wa mabao 5-2 kwenye nusu fainali dhidi ya Ufaransa na mabao mawili zaidi kwenye ushindi wa 5-2 dhidi ya Sweden kwenye fainali.
Hilo lilikuwa taji la kwanza kati ya matatu ya Kombe la Dunia kwa Pele.
Pia alihusishwa kwenye mechi mbili mwaka 1962, kabla ya majeraha kumuacha nje.
Mwaka 1970, akiwa kwenye kiwango chake bora, alifunga mara nne ikiwemo bao la kwanza la Brazil katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Italia.
Mario Kempes, Argentina – 1978
Argentina imeshinda Kombe la Dunia mara mbili na katika matukio yaliyojiri, mchezaji mmoja alitoa mchango mkubwa kwenye mafanikio yao mwaka 1978, katika ardhi ya nyumbani, Mario Kempes.
Mshambuliaji huyo wa Valencia alienda kwenye michuano hiyo akitoka kutwaa kiatu cha dhahabu kwenye La Liga katika misimu miwili mfululizo na alikuwa mchezaji pekee kwenye kikosi cha Argentina ambaye hakucheza nchini kwake.
Kempes alishindwa kufunga kwenye hatua ya makundi, lakini baadaye alionesha umahiri wake kwa kufunga mabao yote katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Poland na kisha kufunga bao la kwanza la tatu katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Peru.
Ushindi huo uliipeleka Argentina kwenye fainali na Kempes alifunga mara mbili zaidi katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Uholanzi mjini Buenos Aires, hakuisaidia nchi yake tu kwenye kupata mafanikio ya kwanza, lakini pia alimaliza akiwa mfungaji bora na mchezaji bora wa michuano hiyo.
Paolo Rossi, Italia – 1982
Alienda kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1982 nchini Hispania, mshambuliaji wa Italia, Paolo Rossi akiwa ndio kwanza amerejea uwanjani baada ya kutumikia kifungo cha miaka miwili kwa kashfa ya upangaji matokeo kwenye ligi ya Serie A, huku kocha wa timu ya taifa, Enzo Bearzot akilaumiwa na vyombo vya habari kwa kumchagua kikosini.
Lakini baada ya kuanza kwa kusuasua, mshambuliaji huyo alionesha cheche zake dhidi ya Brazil kwa kufunga ‘hat-trick’ katika mechi ambayo Italia ilishinda na kufuzu nusu fainali.
Ilifuatiwa na kufunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Poland kwenye nusu fainali na kufunga bao la kwanza la Italia katika ushindi wa 3-1 kwenye fainali dhidi ya Ujerumani Magharibi.
Mabao sita ya Rossi yalimfanya kutwaa kiatu cha dhahabu kwenye michuano hiyo.
Diego Maradona, Argentina – 1986
Nahodha Diego Maradona aliongoza kwa mfano mwaka 1986 akiisaidia Argentina kushinda kombe la pili la dunia nchini Mexico.
Bao la kwanza akifunga katika sare ya 1-1 dhidi ya Italia na kuisaidia Argentina kusonga mbele.
Kwenye robo fainali alifunga mara mbili na kuiondosha England kwa 2-1. Bao la kwanza likiwa maarufu kama mkono wa Mungu kwani Maradona alifunga kwa mkono dhidi ya Peter Shilton.
Lakini bao la pili lilikuwa moja kati ya mabao bora ya muda wote kwenye Kombe la Dunia.
Ilifuatiwa na mabao mawili zaidi kwenye ushindi wa 2-0 katika nusu fainali dhidi ya Ubelgiji kisha wakashinda 3-2 kwenye fainali dhidi ya Ujerumani Magharibi.
Akifunga mabao matano na kutoa pasi tano za mabao jina lake likawa kubwa na kushinda kiatu cha dhahabu kwa kuwa mchezaji bora wa michuano.
Zinedine Zidane, Ufaransa – 1998
Kiungo mwenye ufundi mwingi Zinedine Zidane alikuwa kinara wa Ufaransa iliyokuwa mwenyeji wa michuano hiyo mwaka 1998.
Alianza vizuri kwa kutoa pasi ya bao la kwanza kwa nchi yake lililofungwa na Christophe Dugarry katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Afrika Kusini.
Zidane aliendelea kuimbwa midomoni mwa mashabiki baada ya kufunga bao la kuongoza dhidi ya Saudi Arabia, lakini baadaye alioneshwa kadi nyekundu katika ushindi wa 4-0 na kukosa mechi ya tatu ya kundi kati ya Ufaransa na Denmark, pia ile ya ushindi wa 1-0 kwenye dakika za nyongeza dhidi ya Paraguay katika hatua ya 16.
Lakini alirejea kwa mtindo wa aina yake akifunga kwenye mikwaju ya penalti na kuitupa Italia kwenye robo fainali na kisha kusaidia timu yake kushinda mabao 2-1 dhidi ya Croatia.
Kwenye fainali Zidane alifunga mabao ya kichwa mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Brazil na kiwango chake kilimfanya achaguliwe kikosi bora cha michuano. Miaka miwili baadaye alichaguliwa mchezaji bora wa Euro 2000, ambayo Ufaransa pia ilitwaa ubingwa.
Ronaldo, Brazil – 2002
Fainali za mwaka 1998 zilitarajiwa kuwa nzuri kwa mshambuliaji wa Brazil Ronaldo. Hata hivyo, hakupangwa mwanzo na alipopangwa alishindwa kuonesha makali katika mechi waliyofungwa 3-0 na Ufaransa.
Majeraha ya goti yalimfanya kutokuwa vizuri mwaka 1999 lakini akarejea kwenye makali na kuweka historia yake kwenye soka.
Mwaka 2002 kwenye michuano ya Korea Kusini na Japan, Ronaldo ni kama alilipiza kwenye michuano iliyopita, alifunga mabao manane katika mechi saba alizocheza.
Alifunga mabao manne katika mechi tatu za makundi, moja kwenye ushindi wa 2-1 dhidi ya Uturuki na mengine kwenye ushindi wa 4-0 dhidi ya China na mawili kwenye ushindi wa 5-2 dhidi ya Costa Rica. Kisha moja kwenye ushindi wa 2-0 kwenye hatua ya 16 dhidi ya Ubelgiji. Alifunga pia bao pakee kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Uturuki na mabao mawili kwenye 2-0 dhidi ya Ujerumani katika fainali.
Ronaldo alimaliza akiwa mfungaji bora na hakuna mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi tangu hapo, hata kama Messi na Mbappe wako kwenye wakati wao mwaka huu.