MAREKANI, Florida: NYOTA wa Inter Miami, Lionel Messi, amekiri kwamba licha ya kutokuwa tayari kuondoka Barcelona lakini alilazimika kwenda kuanza maisha mapya katika klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa mnamo mwaka 2021.
Messi alikuwa ameichezea Barcelona tangu akiwa na umri wa miaka 13, lakini aliwaacha wababe hao wa LaLiga baada ya mkataba wake kumalizika na kushindwa kuongeza kandarasi mpya.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alifunga mabao 16 na kutoa pasi za goli (asisti) 16 kwenye Ligue 1 msimu wa 2022 – 2023.
“Mabadiliko ya kwenda PSG yalikuwa magumu kwa sababu nilikuwa nafanya vizuri sana Barcelona na sikutaka kuondoka nilipanga nibaki Barcelona.
“Sikuwa tayari kuondoka, kila kitu kilitokea haraka sana, ilibidi niende kujenga upya maisha yangu huko Ufaransa. Nilijua mabaya na mazuri ya ligi nyingine, klabu nyingine na chumba kipya cha kubadilishia nguo.
“Ilikuwa mabadiliko ambayo hatukuwa tunayatazamia na ndiyo maana nilikuwa na wakati mgumu mwanzoni mwa ligi.” Ameeleza Messi.