Meya Ngwada asisitiza uwajibikaji manispaa ya Iringa

IRINGA: Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, ameagiza kuimarishwa kwa uangalizi na usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa kiwango kinacholingana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali.
Akilihutubia Baraza la Madiwani leo mara baada ya kuchaguliwa kwa muhula wa pili kuwa meya wa manispaa hiyo, Ngwada alisema Serikali inawekeza rasilimali nyingi katika miradi ya maendeleo, hivyo ni lazima kila mradi ukamilishwe kwa ubora, kwa wakati na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.

“Hatutaendelea kuruhusu miradi inayotelekezwa bila viwango. Kila senti inayotolewa na Serikali lazima ionekane kwenye matokeo,” alisema Ngwada.
Alisema moja ya vipaumbele vyake katika muhula huu wa pili ni kuhakikisha usimamizi madhubuti, ufuatiliaji na tathmini ya miradi yote ya manispaa unafanyika kwa karibu ili kuondoa mianya ya uzembe na matumizi yasiyo sahihi ya fedha.
Katika hatua nyingine, Meya Ngwada ameahidi kuongeza mapato ya Manispaa ya Iringa kwa kusimamia kikamilifu ulipaji wa kodi na tozo kwa wafanyabiashara na taasisi zote zinazowajibika.

Alisema ongezeko la mapato litawezesha kuboresha huduma za kijamii na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mipya.
“Tukisimamia mapato vizuri, tutajenga miundombinu bora, kuboresha huduma za afya, elimu na kuongeza ajira kwa vijana wetu,” alisisitiza.
Ameeleza kuwa miradi yote iliyoanzishwa itakamilishwa kwa wakati, sambamba na kuanzishwa kwa miradi mipya yenye lengo la kupanua fursa za kiuchumi katika manispaa.
Meya Ngwada pia ametoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi, akiwamo baadhi ya wabunge na watendaji, wanaotuma wawakilishi katika vikao vinavyohitaji uwepo wao binafsi.
Alisema kitendo hicho kimekuwa kikisababisha ucheleweshaji wa maamuzi na kuathiri utekelezaji wa maazimio ya baraza.
Ameitaka pia Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha inahudhuria vikao vyote muhimu ili kuweka uwazi na urahisi wa utoaji wa taarifa zinazohitajika katika maamuzi.
Amewataka watendaji wote wa Manispaa ya Iringa kuongeza uwajibikaji, ufuatiliaji na weledi katika majukumu yao ya kila siku.
“Nataka kuona mabadiliko. Wananchi wanatutegemea. Huu ni wakati wa kufanya kazi kwa umoja na dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo chanya,” alisema.



