MFALME mpya wa Uingereza, Charles III anayeapishwa leo, atawekewa alama maalumu ya kumbukumbu ya ziara yake aliyoifanya ndani ya Hifadhi ya Arusha (ANAPA) zaidi ya miaka 12 iliyopita.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Yustina Kiwango alisema Mfalme Charles III enzi hizo akiwa Mwana wa Mfalme, alivutiwa sana na mti mkubwa aina ya mkuyu uliopo mkabala na maporomoko ya maji ya Tululusia na kwamba ni katika eneo hilo ndipo kibao maalumu cha kumbukumbu ya ziara hiyo kitawekwa.
“Mfalme Charles alikuwa akitalii hifadhini kwa miguu, tofauti na wengine wanaopenda kufanya ziara wakiwa ndani ya magari,” alisimulia Askari Mwandamizi wa Uhifadhi, Michael Ngatoluwa aliyeshiriki kumlinda alipofanya ziara hifadhini hapo.
Ngatoluwa ni mmoja wa watu wachache walioruhusiwa kuandamana na Mfalme Charles na mkewe Camilla Parker. “Jambo la ajabu ni kwamba ingawa Mfalme na Malkia walijionea aina nyingi za wanyama kama tembo, twiga, nyumbu na nyati, hawakuvutiwa na yeyote kati yao hadi walipofika katika maporomoko ya maji na kuuona mti mkubwa wa mkuyu,” alisema Ngatoluwa.
Alisema Mfalme Charles na mkewe walisimama kwa muda mrefu chini ya mkuyu na kuanza kuuliza maswali mengi kuhusu mti huo. “Bahati nzuri kulikuwa pia na wanafunzi wa Chuo cha Wanyamapori cha Mweka, Moshi, ambao walikaribishwa kukutana na hata kuzungumza na Mfalme Charles, hivyo walijibu maswali yake vizuri sana,” aliongeza Ngatoluwa.
Kwa mujibu wa Ngatoluwa, Mfalme Charles na Camilla walishangazwa na ukubwa wa mkuyu uliopo katika hifadhi hiyo, na walisema Uingereza, mikuyu huwa ni miti midogo na mara nyingi huoteshwa na watu katika bustani zao majumbani. Mkurugenzi wa Kampuni ya African Environment, Richard Beaty ndiye aliyeongoza msafara wa Mfalme Charles jijini Arusha Novemba 9, 2011 wakati huo akiwa Mwana Mfalme wa Uingereza.
Miaka miwili baadaye Malkia wa Uingereza, Elizabeth II aliyefariki mwaka jana, alimtunuku Beaty nishani maalumu ya OBE kwa utumishi uliotukuka.
Kabla ya ziara yake ya mwaka 2011, Mfalme Charles III enzi akiwa Mwana wa Mfalme, aliwahi kutembelea Tanzania mwaka 1981, lakini ziara yake ikijikita zaidi katika mikoa ya Kusini. Mama yake Malkia Elizabeth II akizuru Tanzania mwaka 1979 na kupokelewa mkoani Dar es Salaam na mwenyeji wake, Mwalimu Julius Nyerere.
Leo Mfalme Charles III anaapishwa kuongoza Uingereza kutokana na kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth II aliyeaga dunia Septemba 8, 2022. Ataapishwa rasmi leo kwenye Westminster Abbey, na Mfalme ambaye ataapishwa moja na Camilla, Malkia wa Consort, atakuwa mfalme wa 40 kutawazwa tangu mwaka 1066