MFANYABIASHARA na shahidi katika kesi ya kupanga njama za kutenda kosa na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayowakabili watu watatu, Zulfa Rashid ameieleza mahakama alivyotapeliwa Sh 129,881,050.
Washitakiwa ni Selemani Mohamedi, Mohamedi Selemani na Zaituni Selemani na Zufla alitoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu mkazi mkuu, Ramadhan Rugemalila anayesikiliza kesi hiyo.
Akiongozwa na wakili wa serikali, Mosie Kaima, Zulfa alidai kuwa amemfahamu mshitakiwa Selemani Mohamedi baada ya kutambulishwa na wenyeji wake katika Kijiji cha Nanganga mkoani Lindi mwaka 2006 alipokwenda kununua mazao ya ufuta, korosho na njugu mawe kwa ajili ya biashara.
Alidai baada ya kufika Nanganga, wenyeji walimwambia kuwa kama anataka kupata mzigo kwa haraka na urahisi, aonane na Selemeni kwa kuwa ni dalali mwaminifu na hawezi kukimbia na fedha zake kwa kuwa anafahamika na amewekeza kijijini hapo.
Zulfa alidai alimtafuta Selemani akiwa na rafiki yake Mama Angel na walifanikiwa kusaidiwa kupata tani 10 za mazao tajwa na kwenda kuyauza Zanzibar na baada ya hapo hakuwahi kuonana tena na Selemani.
Alidai mwishoni mwa mwaka 2018 akiwa Dar es Salaam, alipokea simu kutoka kwa Selemani akimweleza kuwa kuna ujenzi wa ofisi ya Halmashauri Zanzibar na zinahitajika mbao kwa ajili ya ujenzi huo.
Alidai kuwa Selemani alimwambia atoe Sh milioni 20 kwa ajili ya kwenda kununua mbao na wangepata faida ya Sh milioni 15. Alikubaliana kufanya biashara hiyo na walikutana eneo la bandarini na kumkabidhi fedha hiyo kwa ajili ya kufuata mbao mkoani Lindi.
Zulfa alidai ulipita muda hakukuwa na mrejesho wowote kuhusu upatikanaji wa mbao na mauzo yake na alipompigia aliambiwa kuwa mbao alishaziuza kwa halmashauri hivyo anasubiri mchakato wa malipo ukamilike atampatia fedha yake pamoja na faida.
Aliendelea kudai kuwa alisubiri hadi Juni mwaka 2019 ambapo msimu wa mavuno wa njugu mawe ulikuwa umeanza.
Alidai kuwa alimpigia simu Selemani na kumwambia kuwa anahitaji kununua njugu mawe tani 40 zenye thamani ya Sh milioni 44.5 ili aziuze mwezi wa Ramadhani na alijibiwa kuwa ataenda kumnunulia na kumkusanyia kwa kuwa yeye alikuwa anaelekea mkoani Lindi kwa ajili ya likizo akitokea Zanzibar.
Alidai kuwa alimkabidhi Selemani Sh milioni 20 kwa ajili ya ununuzi wa njugu na baadaye alimtumia Sh milioni 19.5 kwa njia ya simu na alimmalizia kiasi kilichobaki walipokutana. Alidai Selemani alimwambia kuwa mzigo amekwishakusanya na kuhifadhi katika ghala.
Kwa mujibu wa Zulfa, baada ya kumpatia fedha hizo alimpatia tena Sh milioni 20 kwa ajili ya ununuzi wa korosho lakini alipozihitaji hakuzipata kwa sababu aliambiwa kuwa amekwisha ziuza na wanalipwa kwa awamu kwa hiyo aendelee kusubiri.
Aliieleza mahakama kuwa mwaka 2020 alimpatia tena Selemani Sh 43,881,050 kwa ajili ya ununuzi wa ufuta na alimkabidhi Sh milioni 20 mkononi na iliyobaki alimtumia kwa simu.
Alisema baada ya kumkabidhi kiasi chote hicho cha fedha, hakupata mizigo yake wala kurudishiwa fedha kutoka kwa Selemani na alipokuwa akimpigia simu alikuwa anamwambia subiri nitakupigia na kutoa sababu nyingine zilizoanza kumpa wasiwasi.
Alidai kutokana na hali hiyo ilikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi na baadaye Selemani alikamatwa.
Alidai Selemani akiwa kituo cha polisi alikiri kupatiwa fedha na Zulfa na alipotakiwa kumlipa, alisema kuwa hawezi kuzilipa peke yake kwa kuwa alishirikiana na wenzake kuzitumia na baada ya hapo hakujua nini kiliendelea.
Kwa upande wao, washitakiwa wakiongozwa na wakili wa kujitegemea, Ester Simon walikana mashitaka na kuendelea kuwa nje hadi Oktoba 20 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo inadaiwa kati ya mwaka 2018 na 2020 katika Mkoa wa Dar es Salaam washitakiwa walifanya njama za kutenda kosa na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh 129,881,050 kutoka kwa Zulfa Rashid kwa nia ya kufanya biashara huku wakijua si kweli.