Mfanyakazi GGML akutwa ameuawa

MFANYAKAZI wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kitengo cha Ugavi, Mirembe Suleman (43) amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa katwa na vitu vyenye ncha kali.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Berthaneema Mlay amethibitisha leo kutokea kwa tukio hilo na kueleza mwili wake umekutwa mtaa wa Mwatulole mjini Geita.

Amesema taarifa za tukio hilo zimeripotiwa Aprili 26, 2023 majira ya 1:30 asubuhi baada ya mwili wake kukutwa katika maboma ya nyumba alizokuwa anajenga eneo la mtaa wa Mwatulole kata ya Buhalahala.

“Timu yetu ya makachero walifika eneo lile na kubaini kwamba mwili wake umekatwa katwa sehemu mbalimbali na amepoteza maisha. Mwili umechukuliwa na umepelekwa hospitali ya Rufaa ya mkoa.”

Amesema tayari watu wannne wanashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo lengo ni kuweza kubaini wahusika wa mauaji hayo na kupata kiini halisi kilichosababisha umauti wa mfanyakazi huyo wa GGML.

“Taarifa za awali za waliofika eneo la tukio wanasema alikuwa amekatwa sehemu za kichwani, usoni, na mikono yote miwili, ambapo mkono wa kulia ulikuwa umeondolewa kiganja.”

Habari Zifananazo

Back to top button