Mfanyakazi wa ndani mbaroni kwa wizi wa mtoto wa miaka 5
MWANZA: JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mwanamke mmoja, Mariam Jeremia kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa kike, Odeta Julius ambaye kwa wakati anaibiwa alikua na umri wa miaka mitano.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha Polisi Kirumba Agosti 08, 2021 na mwanamke aitwaye ,Beatrice Gabriel miaka 47 mfanyabiashara na mkazi wa Kangae B kata ya Mecco ambapo alitoa taarifa za kuibiwa kwa mtoto huyo.
“Mzazi huyo alidai kuwa mtoto wake aliibiwa kati ya majira ya saa 7-10 ambapo alimtuhumu mfanyakazi wake wa ndani aitwaye Mariam Jeremia 27 kwani alitoweka nyumbani na kwenda kusikojulikana huku akiacha ujumbe wa maandishi kwamba ameenda kupata matibabu na mtoto huyo”…
Alisema
Aidha Kamanda Mutafungwa alisema kuwa uchunguzi wa Jeshi la Polisi ulionyesha kuwa Mariam Jeremia alikuwa Jijini Arusha akiendelea na shughuli zake akiwa na mtoto huyo aliyemuiba Jijini Mwanza ambapo Desemba 06, 2023 makachero wa Jeshi la Polisi walifanikiwa kumtia mbaroni mama huyo akiwa anaishi na mtoto huyo aliyeibiwa Jijini Mwanza.
“Hadi anakamatwa alikua amembadilisha majina yake halisi mtoto huyo na kumwita, Edibinya Cruven Brian na kumuanzisha darasa la kwanza katika shule ya msingi Kitefu iliyopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha mtuhumiwa amekamatwa na anatarajiwa kuletwa Mwanza kwaajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria na mtoto amehifadhiwa katika mazingira salama na utaratibu wa kumrudisha Mwanza ili aungane na familia yake unafanyika” ameeleza Kamanda