Mfaume, Pialali kurudiana Sept.1

Mabondia wawili mahasimu, Iddy Pialali na Mfaume Mfaume leo wamesaini mkataba wa kurudiwa kwa pambano lao linalotarajiwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka huu, tukio lililofanyika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam huku kila mmoja akitamba kumaliza pambano mapema.

Pambano hilo lililopewa jina la King Of The Night linaloteka hisia za wengi kutokana na upinzani uliopo baina yao na kambi zao, linarudiwa baada ya lile la awali lililopigwa Arusha kuvunjika baada ya kutafsiriwa mabondia hao waligongana vichwa vilivyopelekea Pialali kupasuka usoni.

Pambano hilo lililokuwa la raundi 10 lililopigwa Desemba 26, mwaka jana na lilivunjika raundi ya kwanza.

Hata hivyo mara baada ya kuingia mkataba huo, Mfaume alitamba kuwa atahakikisha anamchakaza mpinzani wake na kama haitakuwa hivyo basi ataacha mchezo wa ngumi.

“Tusiangalie yaliyopita ilikuwaje, Watanzania wote waliona kilichotokea, hakuna kichwa ni uoga tu, sasa siku hiyo kukimbia hakuna. Mama Mfaume amesema mwanangu ‘kaza buti’.

“Tangu niko mdogo, mama yangu ananiambia hivyo, maana yake pambana, fanya mazoezi kwa bidii halafu kasema raundi ya tatu mwisho, Bi Mkubwa nimenuukuu kauli yako, huyu asipoamkia ICU (chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum), naacha boxing.

“Mama Mfaume kaongea na timu yangu timu ya Mabibo siongei sana, nasemaje tupigane mpaka mmoja afe,” alisema Mfaume.

Naye Pialali alisema: “Mapepe, muoga anatetemeka tetemeka, mwanaume anaongea sana? Mwanaume haongei sana. Nasema niko, safi niko salama, Mfaume safari hii kazi anayo, huyu (Mfaume) ni kondoo sio bondia sasa huyu kondoo dawa yake nishaipata tayari, kuna watu anawategemea lakini huyu kondoo nampiga ‘KnockOut’ mbaya sababu sio bondia, hamalizi huyu hana maajabu.

“Mfaume kampiga nani hapa Tanzania? Sisi tunacheza ngumi hatuogopi, kazi anayo, Manzese msiwe na presha, hapa anajikaza tu ila tutampiga,” alisema Pialali.

Habari Zifananazo

Back to top button