Mfuko wa Faida wazidi kunoga
MFUKO wa Faida unaosimamiwa na Watumishi Housing Investment (WHI), umeongeza faida kutoka Sh bilioni 12 Januari mwaka huu hadi Sh bilioni 15.
Pia thamani ya vipande vya uwekezaji imeongezeka kutoka Sh 100 za wakati huo hadi Sh 103.42, huku idadi ya wawekezaji ikiongezeka hadi kufikia 7,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Dk Fredy Msemwa amesema kuwa ukuaji huo unamaanisha kwa mwaka wanaweza kufikia zaidi ya asilimia 10 hadi 11 kutoka asilimia nne ya sasa.
“Sisi Watumishi Housing tunaendelea na jukumu tulilopewa na serikali la kuwawezesha watumishi wa umma kuwa na makazi mazuri na kwa gharama nafuu na wakati huo huo kupitia kazi yetu ya usimamizi wa uwekezaji tunawawezesha Watanzania kuwa na uwezo wa kiuchumi kupitia uwekezaji katika Faida Fund,” amesema Dk Msemwa.
Ameeleza kuwa kinachosababisha mfuko huo ukue kwa kasi ni weledi unaotumika katika uwekezaji na umakini katika kuchagua sehemu za kuwekeza sambamba na matumizi ya teknolojia na usalama ambayo yamepunguza gharama za uwekezaji.
Pia amesema kupitia uwekezaji huo, WHI inaongeza mtaji wa kujenga nyumba za watumishi wengi na kwamba mpaka sasa wamejenga nyumba 983 katika mikoa 19.
Ameeleza kuwa miradi inayoendelea kwa sasa ni wa nyumba 1,000 uliopo jijini Dodoma, kati ya nyumba hizo, nyumba 203 zimeshauzwa na katika jiji la Dar es Salaam mradi wa Kawe utaanza Julai mwaka huu.
Amesisitiza kuwa katika miradi hiyo wanategemea kuhudumia watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya jamii ili wawauzie nyumba kwa gharama nafuu.