NCHI za Afrika Mashariki zimeanzisha mfumo maalumu wa kukabiliana na majanga unaojulikana kama East Africa Hazards Watch (EAHW) unaolenga kutoa tahadhari mapema kuhusu ukame, vimbunga, nzige wa jangwani, mvua kubwa na majanga mengine yanayotokana na hali ya hewa.
Mfumo huo unaosaidia kupata taarifa za hali ya hewa kwa kusoma ramani, umeanzishwa mwaka mmoja uliopita na umesaidia kutoa taarifa kwa watunga sera ili kuchukua hatua kukabiliana na majanga.
Mtaalamu kutoka Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa na Ongezeko la Joto (ICPAC) kilicho chini ya Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) aliyeshiriki kutengeneza na kuendesha mfumo huo, Eric Otenyo, alisema hayo katika mafunzo maalumu kwa wadau wa masuala ya hali ya hewa yaliyofanyika Nairobi, Kenya.
Mafunzo yaliwakutanisha wataalamu kutoka serikalini, sekta binafsi na waandishi wa habari wa Kenya na Tanzania.
Otenyo alisema kwa kutumia setelaiti, wanaangalia anga ikiwemo baharini kubaini majanga mbalimbali yanayoweza kutokea na kutoa taarifa ya tahadhari.
Kwa mujibu wa Otenyo, tangu kuanzishwa kwa mfumo Julai 2021, kumekuwa na mafanikio makubwa kwa kutoa taarifa zilizotumika katika nchi hizo na kuwezesha kukabiliana na majanga. Umekuwa ukitumiwa na nchi zote za Afrika Mashariki.
Kuhusu hali ya ukame, alisema wanaangalia katika siku 10 kwa kutumia setelaiti ikiwemo kukosekana kwa mvua na kiwango cha maji ardhini na kutaarifu mamlaka za nchi za EAC kukabiliana na ukame.
“Kwa kutumia mfumo huu, tunatoa utabiri wa hali ya hewa kwa siku na katika msimu na kuusambaza kwa wakala wa hali ya hewa kwa kila nchi na kuangalia mvua kama ni nyingi au kawaida, joto, mabadiliko ya hali ya hewa, historia ya eneo husika na vimbunga katika maeneo ya Pwani,” alisema.
Alisema mfumo huo ukizingatiwa na wadau wote, utasaidia kuepuka maafa na kupunguza madhara.
“Tumewafundisha wadau kutumia mfumo huu kuwezesha kuangalia mtandaoni na kutoa taarifa kwa jamii kwa kushirikiana na mamlaka za nchi husika na kufika kwa serikali na watunga sera ili kuchukua hatua stahiki,” alisema Otenyo.
Ofisa Programu wa taasisi ya Foundation for Energy Climate Environment, Euster Kibona, alisema mfumo wa EAHW umekuja wakati sahihi kwani baadhi ya maeneo yakiwamo ya Tanzania hupata mvua mara mbili kwa mwaka huku mengine yakipata mara moja kwa mwaka.
Alisisitiza kuwa, taarifa za tahadhari za mapema ni muhimu kwa nchi ili kujiandaa na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Meneja Uhusiano kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Monica Mutoni amesema shirika lao limekuwa likiwajengea waandishi wa habari kuhusu uelewa zaidi wa mabadiliko ya tabianchi.
“Hiyo imesaidia taarifa za hali ya hewa zikiwemo tahadhari za majanga kufika kwa wananchi kwa wakati katika mikoa yote hasa zile redio za jamii mbalimbali,” alisema.