Mfumo kupunguza unyanyapaa wazinduliwa

DAR ES SALAAM: Utafiti wa Afua ya Mfumo Jumuishi kwa Watoa Huduma za Afya ili kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ikimwi na Watumiaji wa Dawa za Kulevya umezinduliwa leo Machi Mosi, 2024.

Akizungumza Mhadhiri na Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas), Dk Jessie Mbwambo amesema tangu ukimwi ulipogundulika wagonjwa wa ukimwi wamekumbana na unyanyapaa na ubaguzi kitu ambacho ni kikwazo katika jitihada za kidunia kwenye kinga, tiba na huduma nyingine kwa waathirika.

“Kwa mujibu wa Malengo Endelevu ya Dunia  hadi kufikia 2030 inategemewa kudhibiti na kutokomeza Ukimwi, licha ya jitihada mbali mbali tatizo la unyanyapaa limeendelea kwua sababu kuu ya kutofikia malengo hayo,”amesema Dk Jesse

Advertisement

Amesema, Afua ya Mfumo Jumuishi ilibuniwa ili kupunguza unyanyapaa kwa WAVIU katika maeneo ya kutolea huduma za afya.

Amesema Afua hiyo iliyozinduliwa inatarajiwa kutekelezwa katika nchi tatu za Tanzania, Ghana na Zambia ambapo itatekelezwa kwa kutoa mafunzo ya kupunguza unyanyapaa kwa WAVIU katika kada zote za watoa huduma kwenye vituo vya afya, wanafunzi wa vyuo shirikishi na makundi mbali mbali katika jamii.

Nae, Mkuu wa Programu na Uimarishaji wa Mifumo ya Afya kutoka Wizara ya Afya Dk Catherine Joackim, akizindua utafiti  huo amesema  licha ya jitihada mbali mbali unyanyapaa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya zinachangia kutofikia lengo la dunia kutokomeza ukimwi ifikapo 2030.

Amesema, kwa mujibu wa ripoti ya kimataifa iliyotolewa na Shirika la Kupambana na Ukimwi, linaonyesha kumalizika kwa Ukimwi ni utashi wa kisiasa  wa nchi husika.

“Utafiti wetu wa 2022/2023 uliozinduliwa Desemba Mosi mwaka jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ulionyesha watu waliopima na kujua hali zao ilikuwa ni asilimia 83, watu wanaotumia dawa ni asilimia 94.

“Tuna kazi kubwa ya kuelimsiha jamii kutambua afya zao, hasa katika makundi ya watoto, wasichana na wanaume balehe,”amesema.

Amesema pia kuna makundi maalum ikiwemo watumiaji wa dawa za kulevya, na wafanyabiashara wa ngono kuwa ni makundi yaliyoachwa nyuma kutokana na unyanyapaa hivyo kuchangia ongezeko la watu kutopima na kutambua afya zao.