MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeanzisha mfumo mpya wa manunuzi wa kielekroniki National e-Procurement System of Tanzania (NeST) utakaosaidia kudhibiti rushwa, mchakato wa zabuni kuchelewa na kuongeza uwazi wa zabuni.
Mfumo huo uliobuniwa na kutengenezwa na watanzania wenyewe umeanza kufanya kazi Julai 1, mwaka huu ukichukua nafasi ya mfumo wa awali wa TANePS utakaokoma kufanya kazi itakapofika Oktoba 1, mwaka huu.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imepata mafunzo ya siku mbili ya jinsi mfumo huo unavyofanya kazi huku taasisi mbalimbali za serikali nazo kwa upande mwingine zimeendelea na mafunzo ya mfumo huo yanayofanyika katika chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, mjini Iringa
Akizungumza na wanahabari mra baada ya kamati hiyo ya bunge kumaliza mafunzo hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu PPRA, Eliakim Maswi amewataka wafanyabiashara wote kuomba zabuni kwa kutumia mfumo huo mpya kama wanataka kupata kazi za serikali.
Alisema Rais Dk Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kubadilisha utendaji wa mamlaka hiyo na anataka itoke mahali ilipo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo matumizi ya mifumo ya kielektroniki kuleta tija na ufanisi unaostahili.
Alisema taasisi zinazosimiwa na Msajili wa Hazina na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, zinapaswa kuanza kutumia mfumo mpya kwa shughuli za ununuzi wa umma na kwamba itakapofika Oktoba Mosi mwaka huu taasisi nunuzi zote za serikali hazitaweza kutuma mialiko ya zabuni katika mfumo wa zamani wa TANePS.
Awali Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge, Daniel Sillo alisema ni jambo la kupongeza kwa serikali kutenga fedha kwa ajili ya kutengeneza mfumo huo kupitia vijana wa kitanzania ambao ni wabobezi wa katika fani hiyo.
Aliipongeza pia PPRA kwa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria mpya ya manunuzi.
“Hivikaribuni bunge lilipitisha sheria mpya ya ununuzi inayoondosha changamoto zilizokuwepo kwenye sheria ya zamani kwahiyo kwa sheria mpya na mfumo mpya nchi inakwenda kuondokana na changamoto za manunuzi ya umma yaliyokuwa yanatofautiana kwa kiwango kikubwa na bei halisi ya sokoni,” alisema.
Alisema asilimia 70 ya bajeti ya serikali inatumika kwenye ununuzi kwahiyo panapokuwepo na sheria na mifumo mizuri fedha za serikali zinatunusurika.
Aliitaka serikali kutokuwa na msamaha kwa mtumishi wa umma atakayekwenda kinyume cha utaratibu wa manunuzi ya umma.
“Tunatarajia mfumo huu utaongeza uwazi katika ununuzi wa umma, usimamizi mzuri wa fedha za umma, kudhibiti vitendo vya rushwa, ufuatiliaji kukidhi sheria, uwajibikaji na udhibiti wa manunuzi,” alisema.