Mfumo watengenezwa kudhibiti maudhui
TANZANIA imetenga fedha kutengeneza mfumo kudhibiti maudhui yasiyofaa zikiwamo picha za ngono ili kulinda mila, utamaduni wa Mtanzania na makuzi ya watoto.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema hayo juzi usiku alipozungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Nape yuko London kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Mawasiliano ya Jumuiya ya Madola (CTO) kujadili changamoto na fursa zilizoko katika sekta ya mawasiliano.
Akizungumzia hatua ya nchi kutenga fedha kutengeneza mfumo wa kuzuia wananchi kuangalia picha za ngono, Nape alisema hatua hiyo imekuja kutokana na tatizo kuwa kubwa sio tu Tanzania, bali duniani na nchi kadhaa zimeshachukua hatua.
“Tatizo ni kubwa na nchi kadhaa zimechukua hatua na sio ngono peke yake, bali maudhui yanayolenga kuharibu tamaduni na mila za kwetu, tunaolenga hasa kuwalinda ni watoto, serikali ina wajibu wa kuwalinda wapate fursa ya kukua, wakifika ukubwani wayakute,” alisema Nape ingawa hakubainisha ni kiasi gani kimeshatengwa.
Alisema watoto wanaona maudhui yasiyo na maadili kupitia simu janja wanazopewa na wazazi kwa nia njema ya kujifunza hasa kuwa na masomo na maarifa ya kujifunza hivyo ni lazima kuwe na udhibiti wa maudhui ili kuwalinda. Alisema kwa kuzingatia mila na tamaduni za Mtanzania si sawa kusambaza picha za utupu kwenye mitandao kwa kuwa hayo ni mambo ya sirini.
“Kupitia humo kwenye hizo picha za utupu watu wengine wanadhalilishwa, kuna udhalilishaji mkubwa unaoendelea na tukiachia ni kuendelea kuidhalilisha jamii yetu,” aliongeza.
Kamishna wa Watoto nchini Uingereza, Dame Rachel de Souza alisema matokeo ya utafiti kwa watoto wenye umri wa miaka tisa, yameonesha kuwa wameanza kuangalia video za ngono mtandaoni.
De Souza alieleza kuwa utafiti huo pia umeonesha robo ya vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 21, waliangalia picha za ngono kwa mara ya kwanza kwenye mitandao wakiwa bado wako shule ya msingi.
“Utafiti huo wa kitaifa ulihusisha watu 1,000 wenye umri wa kuanzia miaka 16 hadi 21 na asilimia 38 ya waliofanyiwa utafiti walikutana na maudhui yasiyofaa ya video za ngono kwa bahati mbaya kwenye mtandao,” alisema Rachel de Souza.
Nchini Tanzania, kanuni mpya ya maudhui mtandaoni zimeanza kutumika na zimeweka mambo 10 yaliyozuiwa kuchapishwa mtandaoni ikiwemo maudhui ya uongo, unyanyasaji, ukahaba, ngono, mapenzi ya jinsi moja, picha za utupu na uhalifu wa kingono.
Aidha, kanuni hizo zilizotungwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta pia zinazuia kuchapisha au kutangaza habari zinazoingilia faragha ya mtu au utu wa mtu.