Mallorca, HISPANIA; JENGO la ghorofa mbili katika kisiwa maarufu cha utalii nchini Hispania cha Mallorca limeporomoka na kuua watu wanne na kujeruhi watu 21.
Jengo hilo, ambalo lilikuwa na mgahawa, liliporomoka katika eneo la Playa de Palma, Kusini mwa mji mkuu wa Kisiwa cha Mediterania, Palma de Mallorca.
Taarifa ya huduma za dharura zilieleza kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba watu saba kati ya waathirika walikuwa katika hali mbaya na wengine tisa walikuwa na majeraha makubwa na wanatibiwa katika hospitali tofauti.
Msemaji wa Polisi wa eneo hilo, alikiambia kituo cha Redio cha RNE kwamba jengo hilo limeporomoka huenda kwa sababu ya uzito kupita kiasi, lakini sababu halisi bado inachunguzwa.
Televisheni ya umma ya Visiwa vya Balearic, IB3, ambako Mallorca iko, iliripoti kwamba kulikuwa na watu wakicheza kwenye sakafu ambayo ilianguka juu ya sakafu iliyo chini.
Waziri Mkuu wa Hispania Pedro Sanchez alitoa salamu zake kwa familia za waathirika kupitia ukurasa wa mtandao wake wa X, akisema alikuwa “akifuatilia kwa karibu kuhusu ajali hiyo”.