SERIKALI imetangaza mgao wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kwa sababu za kupungua kwa vyanzo vya maji vya Mto Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Akitangaza mgao wa maji leo Oktoba 25, 2022, mara baada ya kutembelea vyanzo hivyo vya maji, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema taarifa aliyopewa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) ni kwamba vyanzo hivyo vimeshuka uzalishaji maji kutoka lita milioni 466 kwa siku, hadi lita milioni 300 sawa na asilimia asilimia 64.
Amesema tatizo la mgao wa maji ni matokeo ya kiangazi kilichosababishwa na kukosekana kwa mvua za vuli, jambo lililosababisha kushuka kwa kina cha maji kwenye vyanzo hivyo.
“Kamati za Ulinzi na Usalama Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro zilishatekeleza wajibu wa kudhibiti uchepushaji wa maji, hivyo asitokee yeyote akasema mvua zinaletwa na serikali au zinaletwa na sera ya Chama Cha Mapinduzi, mvua ni kudra za Mwenyenzi Mungu na hakuna makusudi yoyote kwamba maji yakosekane,” amesema Makalla
Kutokana na changamoto hiyo, Makalla ametoa wito kwa wananchi kutumia vizuri kiasi cha maji yanayopatikana na kufanya maombi, ili mvua za vuli zinyeshe.
Ameiagiza Dawasa kuharakisha mradi wa visima vya maji Kigamboni, ambao utazalisha lita milioni 70, ili kupunguza adha ya maji kwa wakazi wa Kigamboni, Temeke na katikati ya mji.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja amesema Dawasa itatangaza ratiba ya mgao wa maji muda wowote kuanzia sasa.