Mgeta ya miaka 1970 ‘imejivuruga’, jukwaa lataka mabadiliko

KIASI cha meta 2,200 toka usawa wa bahari, maeneo ya Magharibi ya Lukwangule, umbali wa kilometa 40 kutoka Mkoa wa Morogoro inapatikana Tarafa ya Mgeta. Wakazi wake ni Waluguru. Mgeta ni tarafa ya uwanda wa juu katika Wilaya ya Mvomero ikiwa na Postikodi namba 67321.

Ni sehemu inayosifika kwa kilimo cha mboga na matunda ikiwamo njegere, maharagwe, mahindi, magimbi na viazi mviringo.

Mgeta ya miaka ya 1970 iliyokuwa na ubaridi mkubwa ikitiririsha maji mengi matamu na mazingira yenye ukijani kwa sasa ina matatizo makubwa ya mazingira hasa kukosekana kwa miti na pia kupungua kwa maji katika vyanzo vyake.

Kwa kuwa vyanzo vya maji katika eneo hili la Lukwangule tegemeo pia kwa wakazi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, mazingira yaliyoharibika katika tarafa hii hayawezi kusaidia uhakika wa uwapo wa maji kwa mikoa tajwa kwani tayari Mgeta yenyewe ina ugomvi mkubwa wa maji kwa ajili ya shughuli za bustani.

Ukitoka Morogoro kuelekea Mgeta kilometa 20 tu unaanza kupanda taratibu na kuanza kuona maeneo ambayo yalipaswa kuwa na miti ya miyombo haipo na unapoingia langoni (Kidiwa) ile hali ya baridi na harufu ya miti ya miaka ya 1970 haipo na unapokewa na harufu ya joto.

“Kidiwa ikitengwa kuwa eneo la msitu itapendeza sana, naamini ile hali ya hewa ya ubaridi iliyopotea itarejea..‘tumemiss’ ile hali ya ubaridi pale juu utadhani pamewashwa AC halafu kulikuwa na kaharufu fulani hivi cha miti ya mimaidini,” anasema mmoja wa washiriki katika mjadala mkali wa nini kifanyike kurejesha Mgeta ya kijani uliofanyika Jumanne wiki hii kupitia jukwaa la Mgeta, katika mtandao wa kijamii wa Whatsapp.

Pamoja na juhudi ikiwamo kuwapo na tamasha lenye miaka minane linalohimiza uhifadhi wa mazingira la Tamasha la Juu Afrika, bado Mgeta haina ukijani na maeneo machache yaliyobaki ya misitu nayo ikivamiwa kutokana na uwingi wa watu na mahitaji ya shughuli za kibinadamu.

Vita ya mazingira pengine inaonekana haina maana, lakini mahitaji ya binadamu ili yaweze kufanikiwa kama maji na chakula utunzaji mazingira hasa kuwezesha mvua na kutunza vyanzo vya asili vya maji, kama kusipokuwa na utaratibu kazi iliyofanywa na wazee ya kutunza mazingira kwa miaka 400 inaweza kuwa haina maana.

Diwani Batho wa Kibaoni ameonesha njia katika kukabiliana na hali mbaya ya vipara katika maeneo mengi ya kata yake kwa kushawishi upandaji miti na sasa inakwenda vyema.

Mchangiaji wa namna ya kuipa Mgeta uhai alisema kwa uchungu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na upungufu wa maji, Ng’atighwa Cleophace alitolea mfano Mto Mzinga unaopita Langali na kwenda kuungana na Mto Mgeta kwenye miaka ya 80 ulikuwa mto mkubwa ambao walevi wengi hawakuvuka, lakini sasa ni mfereji fulani ukisubiri msimu wa mvua.

Deograsia Chuma anayetekeleza mradi wa miti kwa kata za Mgeta kupitia shirika lisilo la kiserikali la Agriwezesha anahitaji ushirikiano zaidi kutokana na hali ya sasa kutokuwa sawa kufuatia uharibifu mkubwa wa misitu, watu wakikata miti kwa ajili ya nishati huku hakuna miti mingine inayopandwa.

Ingawa ajenda ya utunzaji wa mazingira ni ya kitaifa na dunia kwa ujumla huku serikali ikiwa sikivu na kutoa ushirikiano kwa asilimia kubwa kwa kuunga mkono juhudi za wananchi katika shughuli za maendeleo, kuna kila haja ya kuiangalia Mgeta ambayo kwa sasa ni tegemeo la maisha ya wakazi wa huko na pia maeneo mengine ya taifa.

Kutokana na haja ya uharaka wa kuiboresha Mgeta washiriki wa mdahalo walipendekeza juu ya Afrika kushirikiana na Agrowezesha katika upande wa elimu itakayotolewa kwa njia ya ubunifu unaoakisi utamaduni ili watu wabadilike, waelewe kwa nini wazazi wetu walipanda miti na kufurahia kazi hiyo wakituachia neema tele.

 

Unaweza kushangaa kwa kukosa elimu hata miti iliyopo katika vitalu vinavyosimamiwa na Agriwezesha ambayo ipo tayari kwa ajili ya kwenda shambani isiende au ikienda isitiliwe maanani, kuna haja ya sheria ndogo za kufanya yasiyowezekana kwa kukosekana elimu yaweze kurekebishwa.

“Maguruwe kuna zaidi ya elfu arobaini na kwa kiasi kipindi cha masika chini ya diwani wa Bunduki tulipanda pembezoni mwa barabara kutoka Bunduki kuelekea Maguruwe. Pia tuna kiasi cha miti kwenye kitalu chetu cha ofisi kuu hapa Sanga Sanga ya matunda na mbao pia,” anasema Deograsia katika mhadhara huo.

Jiografia ya Mgeta kama tarafa iko tofauti pamoja na kuwa na maeneo yenye baridi yapo yenye joto hivyo hata katika kufanya ukijani kuna haja kubwa ya kuangalia aina ya miti iwe ya matunda au ya mbao, lakini muda ni sasa.

Kama miti ikijazwa Kidiwa na maeneo mengine ambayo si mashamba na si makazi, si tu itaipendezesha Mgeta lakini pia itakuwa na mvuto wa aina yake kwa watu wanaopenda asili.

“Mimi binafsi nilishiriki katika Mradi wa Mwalimu wangu wa kutumia sanaa za maonesho kuhamasisha watu kupanda miti. Hiyo ilikuwa 1998. Tulikuwa tunasema: Tuhande mibiki inoga (tupande miti).  Tuliweka kambi Nyandira tukiwa na Mzee wangu Mkwidu (yule wa kijijini pale) na akina mama kadhaa wakiwemo mamangu Mama Kurinyangwa na vijana wawili watatu kutoka Tchenzema.

“Wazo lilikuwa tunapozungumzia miti si lazima utenge ekari moja nzima au vipi kwa ajili ya kupanda miti. Wazo lilikuwa kuhamasisha watu kupanda miti katika sehemu mbalimbali kama kwenye maeneo ya nyumbani, kwenye mipaka ya mashamba, kandokando ya barabara.

“Mwalimu wangu alikuwa anasema miti hiyo iliyopandwa kwa kutawanyika huko, ukiikusanya ni sawa na msitu tayari. Kwa hiyo ni kuhimiza watu kupanda miti isiyoleta athari hasi kwa mazao au kwa makazi ya watu. Na wakati ule tuliwakuta pale Nyandira tayari wana vitalu vyao. Tulifanya hamasa hiyo pale Nyandira, Tchenzema, Bumu Lusungi, Gole, Lolo na Pinde. Miaka mingi,” anasema mchangiaji aliyejitambulisha kwa jina moja Chosolwa.

Katika mada ya mazingira pekee washiriki walikuja na maazimio zaidi ya 20 ya kuiwezesha Mgeta wakiitaka serikali kuingilia kati na pia wananchi kutambua mustakabali wao wa kuendelea kusihi katika eneo hilo linategemea wanavyokubali kubadilika na kurudi katika asili, utunzaji wa mazingira.

Waratibu wa jukwaa hilo Jamaica Maghari na Novat Mkandawile wanasema katika kukabiliana na hali mbaya ya mazingira katika tarafa hiyo juhudi za pamoja zinahitajika kwa wadau wote wakiwemo wakazi wa Mgeta, wenye asili, serikali na kila mmoja ambaye anakumbwa na athari ya uharibifu wa mazingira Mgeta.

Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam chanzo cha maji yao ni Lukwangule, pamoja na juhudi ya kutunzwa kwa sehemu ya misitu ya Lukwangule, Mgeta inapokuwa kame, na pembezoni pia kutakuwa na balaa.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
mwanadongo mmaze
mwanadongo mmaze
1 month ago

Kuna kitu kinafaa kufanywa huku ili dar isikose maji kuwa na hatua endelevu kabla hali haijawa haiwezekani

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x