Mgodi Kitalu C wageuka shamba la bibi
IMEELEZWA mgodi wa Kitalu C wa Madini ya Tanzanite uliopo Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara umekuwa shamba la bibi baada ya wafanyabiashara wakubwa watatu kuingia katika mgodi huo na kuvuna madini ya mamilioni ya fedha bila hatua yoyote kuchukuliwa.
Mgodi huo unaomilikiwa na serikali na mbia mwekezaji mzawa kampuni ya Franone.
Kampuni tatu zinazodaiwa kuingia Kitalu C na kuchimba kwa njia haramu maarufu kwa njia ya bomu ni pamoja na kampuni ya Tanzanite Explore inayomilikiwa na Victor Philipo Mkenga na kampuni ya Saniniu Mining inayomilikiwa na Bilionea Saniniu Laizer na Kampuni Manga Gems(T) Ltd inayomilikiwa na familia ya marehemu Mathias Manga.
Akithibitisha tukio hilo Ofisa Mfawidhi wa Madini Mirerani ,Mernad Msengi alisema ni kweli ofisi yake ina taarifa za tukio hilo na hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja kusimamishwa uchimbaji kwa wafanyabiashara hao waliovamia Kitalu C.
Lakini pia kuwapa nafasi ya mazungumzo kati yao na kampuni ya Franone kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
,,Ni kweli tukio hilo lipo na ofisi yangu imeshachukua hatua ikiwemo kusimamisha uchimbaji kwa kampuni zinazomilikiwa na wafanyabiashara hao kusimama na tumewapa nafasi ya mazungumzo kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa.” alisema.
Awali tukio lingine liliwahi kutokea Machi 10 hadi 13 mwaka huu kwa kampuni ya Gem Rock Venture inayomilikiwa na mfanyabiashara Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti kuchimba kwa njia haramu katika kitalu C na kufanya serikali kukosa mapato hivyo hatua zaidi zinahitajika juu ya kuthibiti uchimbaji huo haramu kwa wafanyabiashara wakubwa.
RaisSamia Suluhu Hassan mapema mwaka jana katika hotuba zake aliwahi kuwaonya wafanyabiashara wa Tanzanite kuacha mara moja kuvamia mgodi wa Kitalu C na kuchimba kwa njia ya bomu na kusisitiza kuwa atayekaidi amri hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Habari kutoka katika Mirerani zinadai kuwa wafanyabiashara hao walivamia mgodi wa Kitalu C mwanzoni mwa mwezi huu na waliingia zaidi ya mita 600 katika kitalu hicho na kuchimba kwa njia haramu.
Vyanzo vilidai kuwa Saitoti alipochimba kwa njia haramu katika mgodi wa Kitalu C serikali ilimchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kumfungia mgodi wake na pia alifikishwa mahakamani kujibu mshitaka lakini kwa wafanyabiashara hao imekuwa tofauti hivyo kuonyesha wazi kuwa wafanyabiashara hao wanalindwa na baadhi ya vigogo wa serikali kama wanavyotamba wao.
Mkurugenzi wa Manga Gems, Brayan Manga alipoulizwa juu ya tukio hilo alijibu kwa dharau na kusema kuwa hana taarifa za kuvamia kitalu C na kusema kuwa hakuna mtaalamu aliyethibitisha kuwa yeye amevamia mgodi huo.
Mfanyabiashara Victor Mkenga na bilionea Saniniu Laizer kupatikana kuelezea tuhuma hizo kwa kuwa simu zao za kiganjani zilikuwa zikiita bila ya kupokelewa pamoja na kutumiwa ujumbe wa sms mara zote bila ya mafanikio lakini juhudi zaidi zinaendelea kuwasaka.