Mgodi ulioua 8 Geita kurasimishwa
NAIBU Waziri wa Madini Dk Steven Kiruswa, ameagiza mmiliki wa leseni ya utafiti wa eneo la mgodi uliosababisha vifo vya watu nane wilayani Geita kuhakikisha anakamilisha tataribu za kupata leseni ya uchimbaji, ili mgodi huo urasimishwe.
Maafa hayo yalitokea Machi 10, 2023 katika Kijiji cha Igando, Kata ya Magema wilayani humo, baada ya watu tisa kuvamia na kuanza kuchimba madini eneo hilo bila kufuata utaratibu na baadaye mashimo hayo kujaa maji ya mvua.
Dk Kiruswa ametoa maagizo hayo leo wakati akizungumuza na wananchi baada ya kutembelea eneo hilo na kuelekeza ofisi ya madini mkoa kusimamia urasimishaji huo, ili kuruhusu shughuli za uchimbaji zifanyike kwa usalama.
“Hii siyo dhamira ya serikali kuona watu wanachimba kiholela, ndiyo maana sheria zimetungwa, ndiyo maana kanuni zimewekwa, na jambo kama hili linapotokea tuna kila sababu, kuhakikisha kwamba halitokei tena.
“Naiagiza Tume ya Madini waje hapa watoe semina wananchi hawa waelewe, sheria ya madini inasema nini na kanuni zake zinasema nini, kuhusu utaratibu wa mtu anapotaka kuchimba madini, anatakiwa apitie hatua zipi,” amesema.
Amewataka viongozi wa vitongoji, vijiji na kata kuhakikisha wanatoa taarifa mapema kwenye mamlaka husika wanapona dalili za uchimbaji holela, ili kuepusha majanga mengine kuweza kujitokeza.
Amewaonya wananchi kuacha kuendekeza uchimbaji holela badala yake waheshimu sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji wa madini ili shughuli zifanyike kwa tija katika mnyororo mzima wa thamani.