Mgodi wakusudia kupunguza eneo ililotaka
MPANGO wa kupanua wigo wa uwekezaji katika mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara, uliyopo Nyamongo, Tarime, mkoani Mara umeendelea kukwama na sasa mgodi huo umekusudia kupunguza eneo kutoka ekari 378, hadi 57 zilizokusudiwa kutwaliwa katika Kijiji cha Kewanja.
Mthamini kutoka Wizara Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rashid Mageta, amesema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee, aliyetembelea Mgodi huo jana na kutaarifiwa juu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Barrick North Mara.
Alitaja sababu kuwa ni fedha za kulipia fidia eneo hilo kufika Sh Bilioni 21, hivyo mgodi umeiandika barua wizara hiyo ikielezea kusudio lake hilo, lakini bado haijajibiwa.
“Kiini cha yote haya ni tegesha (wenye maeneo kuongeza nyumba na mazao, baada ya zuio) kwa madhumuni ya kulipwa fidia kubwa,” alisema Mageta.
Alitoa mfano, wakati wakifanya uthamini eneo hilo walikuta shamba lenye mita za mraba 3658.
488 (pungufu ya eka moja) limeoteshwa miti 3,421 (miti maji 2,987 na miti ya aina nyingine 434), wakati kitaalamu eka moja hutakiwa ioteshwe miti isiyozidi 640.
Maelezo hayo yalimshangaza Meja Jenerali Mzee aliyehoji maana ya kufanya uthamini, kwa sababu kwa ufahamu wake katika mazingira hayo, ilitakiwa itambuliwe miti inayostahili kuoteshwa kwenye eneo husika na siyo vinginevyo.
“Yaani hapo mbona kila kitu kipo wazi, inayokubalika kitaalamu ndiyo inayostahili kulipwa, mingine ni sawa na bhangi tu,” alisema Meja Jenerali huyo.
Naye Mageta alisema miongoni mwa njia zinazokusudiwa kutumika ili kutatua changamoto hiyo ni pamoja na kushirikisha wataalamu wa kilimo, wabainishe kiasi cha mazao yayostahili kuoteshwa kwa kuzingatia ukubwa wa ardhi katika eneo hilo.