Mgogoro wa ardhi kupatiwa ufumbuzi Mtwara

MTWARA; SERIKALI imejipanga kujadili na kutoa suluhisho la kudumu kuhusu mgogoro wa ardhi baina ya kikosi cha jeshi 665 na wananchi wa Mbae Mashariki, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Stergomena Tax, amesema hayo mara baada ya kutemebelea eneo hilo kwa kutumia helikopta ya jeshi na kujionea namna ambavyo wananchi wamevamia na kuweka makazi ya kudumu kwenye eneo hilo, ambalo linamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa Kwa ajili ya ulinzi na usalama.

Stergomena amewaambia wananchi wa Mbae Mashariki kuwa, suluhisho hilo litatolewa ndani ya mwezi huu wa Machi na kwamba litakuwa ni suluhisho ambalo litazingatia maslahi mapana ya ulinzi na usalama na kwa wananchi wa maeneo hayo.

Advertisement

“Kama nilivyosema, nimepokea taarifa na mimi mwenyewe kutembelea na kulinganisha taarifa zote, tumekubaliana kwamba hizi taarifa tuzichakate na pamoja na tutoe tamko ambalo litakuwa ni suluhisho la kudumu,” amesema.

Tax amesema aliamua kufika kwenye eneo la mgogoro baada ya Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hassan Mtenga kumuomba afike na kujionea mwenyewe namna ambavyo wananchi wamevamia na kujenga ndani ya eneo bila kujali vitahatarishi ndani ya eneo la shughuli za jeshi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mtenga amesema mgogoro huo wa ardhi umedumu kwa muda mrefu, huku juhudi nyingi zikifanyika na kushindwa kuleta suluhisho la kudumu.

Mtenga amesema wananchi wa Mbae Mashariki walivamia na kujenga nyumba na kufanya shughuli zao ndani ya eneo ambalo lilitengwa maalum kwa ajili ya shughuli za jeshi.

Mtenga amesema wananchi hao wamejenga mpaka kufikia karibu na maeneo ambayo yana zana za jeshi ikiwemo rada jambo ambalo linahatarisha usalama wa wananchi hao kiafya.

Katika hatua nyingine, Waziri Tax amewaomba wananchi hao kutathimini na kuchukua hatua kwa ajili ya usalama na watoto kuhakikisha makazi yao na shughuli zao hazifanyiki karibu na zana za jeshi hilo.