KOCHA Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema kuwa wanaenda Kanda ya Ziwa wakiwa na lengo moja la kutafuta pointi tisa ambazo zitawaweka kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kanda ya Ziwa Simba itaanza kampeni ya kuzisaka pointi tisa kwa kuikabili Geita Gold keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kabla ya kuikabili Kagera Sugar siku tatu baadaye na kumaliza na KMC Desemba 26.
Simba wanaoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wako nyuma ya vinara Yanga kwa pointi nne hivyo wanahitaji pointi tisa ili kuongeza mbio za kuwania kombe msimu wa 2022/23.
Mgunda alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kikosi chao kilitarajiwa kuondoka leo asubuhi kuelekea Mwanza na kikosi kamili isipokuwa mchezaji Peter Banda ambaye anasumbuliwa na kifundo cha mguu.
“Wachezaji wote wako fiti na wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zetu za Kanda ya Ziwa, tunaenda kupambana kutafuta pointi tatu kila mechi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya mbio za ubingwa,” alisema Mgunda.